NA MWANDISHI WETU
MAKAMU
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema
ili kujenga Taifa imara, ni wajibu kuweka misingi bora ya kuwaandaa
wasomi wenye weledi watakaoweza kukabiliana na changamoto za mabadiliko
kwa ajili ya zama zijazo.
Mheshimiwa
Othman ameyasema hayo Oktoba 22, 2022, akiwa Mgeni Rasmi wa Ufunguzi wa
Mkutano wa Pili wa Kumuenzi aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa
Zanzibar, Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, huko katika Hoteli ya
Golden Tulip, Uwanja wa Ndege, Mkoa wa Mjini Magharibi unguja.
Amesema
kuwa, wakati huu ambao jamii inaelekea katika mjadala mkubwa wa mageuzi
ya sekta ya elimu, na iwapo kuna umuhimu wa kujenga hatima njema, taifa
imara na kizazi kilichotayarishwa kukabiliana na changamoto za zama
zijazo, ni wajibu kuwa na tafakuri ya dhati, ya wazi na yenye upeo
stahiki.
Mheshimiwa
Othman amesema kuwa ili kuenzi dhamira ya dhati na maono ya Marehemu
Maalim Seif, katika kujenga Zanzibar na Tanzania Mpya, huru, yenye
uchumi imara, amani na maridhiano, safari inaanzia na uhuru katika Sekta
za Elimu na Jamii, zinazojali ukuzaji wa vipaji, ubunifu na uwezeshaji.
Aidha,
Mheshimiwa Othman akieleza umuhimu wa Taasisi ya Maalim Seif sambamba
na Mkutano huo amesema, “Taasisi inatoa fursa muhimu ya kuwaleta
wananchi pamoja na kujadili, kubadilishana mawazo na kuendeleza misingi
ya kitaifa bila kujali itikadi wala misimamo; kwa hakika ni nyenzo
muhimu ya ujenzi wa Taifa”.
Akiwasilisha
Mada kuhusu Mjadala wa Kidunia Juu ya Elimu Sahihi kwa Watoto Werevu,
Mheshimiwa Othman amefafanua kwa kusema, “katika hili ni vyema kueleza
mapema kwamba watoto werevu wamekusudiwa ni wale waliotayarishwa
kukabiliana na changamoto za sasa na tunakoelekea katika maisha kwa
ujumla wake”.
Katika
Mada yake, licha ya kubainisha kuwa suala la ubora wa elimu na watoto
weledi, ni kitendawili kigumu kukitegua, bali yapo mambo ya msingi
ambayo jamii inawafiki kuyazingatia ili kufikia mafanikio zaidi.
Mafanikio
ambayo ni pamoja na Elimu ya Dini, maadili, aina ya wazazi na walezi,
makuzi, mazingira ya kusoma, nafasi na hadhi ya mwalimu, mwanafunzi,
mitaala, mfumo wa usimamizi wa ubora wa elimu na aina ya uchumi wa nchi
kwa jumla.
Pia
utayarishaji wa wanafunzi kuwa na upeo wa kufikiri na kutumia elimu
katika mazingira yao badala ya kukariri; uandaaji wa wanafunzi kuwa
wabunifu; na utayarishaji wanafunzi kuwa na uwezo wa kuwasiliana na
kuwasilisha mawazo yao ikiwemo kutathmini na kuhoji.
Kwa
upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Maalim Seif, Bw. Ismail
Jussa Ladhu, ameeleza kwamba katika Maadhimisho ya Mwaka huu, wameamua
kwenda sambamba na yale aliyoyatarajia Mwanaharakati huyo maishani
mwake, yakiwemo Maudhui Bora ya Elimu.
Naye,
Mwanazuoni na Mwanataaluma Mashuhuri, Profesa Issa Shivji, akitilia
mkazo dhamira ya Marehemu Maalim Seif katika kupigania haki, ameitaka
Taasisi hiyo kumuenzi Kiongozi huyo kwa kuzingatia maono muhimu ya Haki
na Uhuru, katika Sekta za Elimu na Jamii.
Wengine
waliopata fursa ya kuwasilisha Salamu zao za Kumuenzi Marehemu Maalim
Seif, ni pamoja na Balozi Didier Chassot (wa Uswisi katika Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania); Mhe. Regina Hess (Balozi wa Shirikisho la Jamhuri
ya Ujerumani Nchini Tanzania);
Bi.
Inge Herbert (Mkurugenzi wa Eneo la Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara
– ‘Friedrich Naumann Foundation for Freedom’); Jorunn Maehlum (Balozi
Mstaafu wa Norway, Nchini Tanzania);
Bw.
Mark Green (Balozi Mstaafu wa Marekani, Nchini Tanzania); na Bw.
Roeland van de Geer (Balozi Mstaafu wa Umoja wa Ulaya (EU) Nchini
Tanzania), ambao wote wamemkumbuka Marehemu Maalim Seif kuwa Mtu wa
pekee, jasiri, mpambanaji na ambaye hakukata tamaa hadi mwisho wa maisha
yake.
Kaulimbiu
ya Mkutano huo wa Pili, wa Siku Mbili, ambao umeandaliwa na Taasisi ya
Maalim Seif (Maalim Seif Foundation) kwa mashirikiano na Jumuiya mbali
mbali za Kitaifa na Kimataifa, ni Elimu na Ukuzaji Vipaji, Ubunifu na
Uwezeshaji.
Viongozi
wa Serikali, Dini, Vyama vya Siasa, Mawaziri na Mawaziri Wastaafu,
Wasomi na Wanataaluma, wakiwepo pia Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Sheikh
Hassan Othman Ngwali; Wachambuzi wa Siasa za Kitaifa na Kimataifa, Bw.
Ahmed Rajab kutoka Uingereza, Bw. Hamza Kasongo kutoka Dar es Salaam;
Balozi Ali Abeid Karume; Bw. James Mbatia; Wakuu wa Mashirika ya
Kimataifa; Sekta Binafsi; Asasi za Kiraia; na Wanadiplomasia mbali mbali
kutoka ndani nje ya Tanzania, wamehudhuria katika Mkutano huo.
Wengine
waliohudhuria hapo ni pamoja na Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Mhe.
Zitto Zuberi Kabwe; Mjane wa Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, Bi Awena
Sinani Masoud; na Mke wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mama
Zainab Kombo Shaib.
0 Comments