WAZIRI
wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mheshimiwa
Dkt.Dorothy Gwajima anatarajiwa kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika Mashindano ya
Utanashati, Urembo na Mitindo ya Viziwi Duniani ambayo yanafanyika
nchini.
Mashindano
hayo ya 12 duniani yanafanyika leo Oktoba 29, 2022 katika Ukumbi wa
Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam
ikiwa ni mara ya kwanza kufanyika barani Afrika na Tanzania kuwa wenyeji
wa kwanza.
Hayo
yamesemwa Oktoba 28, 2022 jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu
Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt.Hassan Abbas wakati
akizungumza na waandishi wa habari.
Ni
mbele ya Kamati ya Maandalizi ya Mashindano hayo ikiongozwa na Rais wa
Mashindano ya Urembo na Utanashati kwa Viziwi Duniani (MMDI),Bi.Bonita
Ann Leek ambapo Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed
Mchengerwa naye atakuwa mgeni maalumu.
"Mheshimiwa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alikuwa
aungane nasi, lakini kutokana na majukumu mbalimbali, Mheshimiwa Rais
atawakilishwa na Mheshimiwa Dorothy Gwajima, Waziri wa Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu.
"Mashindano
haya sio jambo dogo ni jambo kubwa sana, watu wengi wako hapa na mpaka
sasa Mheshimiwa Rais wetu amekubali jambo hili kubwa kufanyika hapa
nchini kwetu,"amebainisha Dkt.Abbas.
Dkt.Abbas
amebainisha kuwa, Serikali pia imewapa zawadi washindi wote wa shindano
hilo la kidunia na viongozi wao kutembelea mbuga ya wanyama ya
Ngorongoro Oktoba 31,2022 baada ya kumalizika kwa mashindano hayo kesho
ikiwa ni mwendelezo wa Royal Tour iliyoasisiwa na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Dkt.Abbas
amefafanua kuwa, miongoni mwa sababu zinazoendelea kuifanya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kuendelea kuaminika na kupewa kipaumbele katika
masuala mbalimbali duniani achilia mbali ukarimu, umoja na upendo ni
pamoja na utulivu na amani ambayo imetawala kila mahali.
Pia
amesema, Tanzania imebarikiwa kuwa na vivutio mbalimbali kuanzia Bara
na Visiwani ambavyo kila mgeni akivisikia anatamani kufika ili kuja
kufurahia maisha.
"Hapa
Tanzania tumejaliwa kuwa na vivutio vingi kuna Serengeti, Ngorongoro,
Zanzibar na maeneo mengine mbalinbali ya vivutio vizuri vya kwenda
kurelax. Kwa Tanzania tangu mashindano haya yaanze kufanyika, Tanzania
ni nchi ya 12 na kwa mara ya kwanza mashindano haya yalifanyika Las
Vegas nchini Marekani mwaka 2010,"amesema.
Amesema,
tukio hilo ambalo linatarajiwa kufuatiliwa na mamilioni ya watu ndani
na nje ya nchi litawakusanya pamoja wageni zaidi ya 1,400 ukumbuni hapo
na litarushwa kupitia vyombo mbalimbali vya habari huku likisindikizwa
na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali.
"Na
niwaambie tu, katika tukio hilo itaanza kuoneshwa filamu ya Royal Tour
iliyochezwa na Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan ili watu waweze kuona jinsi
Tanzania ilivyobarikiwa kuwa na vivutio mbalimbali vya utalii,"ameeleza
Dkt.Abbas.
Serikali inajali
Wakati
huo huo, Dkt.Abbas amesema,Serikali itaendelea kukuza vipaji na vipawa
mbalimbali walivyonavyo watanzania, pili kuheshimu na kulinda na
kuendeleza vipaji na vipawa vya Watanzania wenye changamoto mbalimbali
za ulemavu.
"Pia
tuna sheria za nchi zinawalinda, kutunza haki zao na tuna sera, majengo
yanayowawezesha kupata huduma na mikakati mbalimbali imewekwa na
Serikali yetu ili kuwapa nafasi kwenye nyadhifa mbalimbali za uongozi.
"Kwa
hiyo Serikali inaendelea na juhudi mbalimbali za kuwaunga ndugu zetu
hawa mkono. Mnafahamu kuna timu yetu ilienda mpaka Uturuki ikashiriki
michezo ikafika mpaka robo fainali na wameitangaza Tanzania vyema
duniani. Kwa wale wanaoshiriki michezo Serikali inawasapoti sana, viziwi
pia Serikali inawasapoti sana kwa kila hatua njema.
"Kule
Uturuki, tulianza kucheza na Hispania tukatoana nao bila kwa bila,
tukacheza na Poland kwa tabu sana wakatufunga 3-0, akaja Mjapan
tukamtandika bao 2, wakaja Waitaliano tukawapiga, Mwenyezi Mungu wa
ajabu sana na ni mwingi wa rehema. Kuna wenzetu wazima, lakini hawawezi
kufanya mambo makubwa kama haya. Kwa hiyo Serikali itaendelea kuwaunga
mkono,"amefafanua.
Lugha ya alama
Katibu
Mkuu Dkt.Abbas amesema, "Lugha ya alama ni jambo ambalo Serikali kwenye
programu zake mbalimbali imekuwa ikilifanya ili kuwasaidia wenzetu
waendelee kuwasiliana na katika vyuo vikuu kuna programu kabisa wenzetu
wanasoma.
"Wataalam
kila mwaka wanakuja kusaidia, wameweka departments (idara) au units
(vitengo) kabisa za special needs (wenye mahitaji maalumu), special
education (elimu maalumu) kadri tunavyozidi kuwabaini na Mheshimiwa Rais
kesho kutwa atatangaza matokeo ya Sensa...itakuja kusaidia kujua viziwi
wangapi ili kuongeza idadi ya wataalam," amesema.
"Hata
sisi kwenye haya mashindano tulitaka wakalimani...kwenye lugha ya alama
wapo wakalimani wa Kimataifa na wakalimani wa Tanzania, jinsia wewe
unavyomwelezea Rais Samia ni tofauti na wanavyofanya Kimataifa.
"Pia
Tanzania tunacreate symbols (alama) zetu na wenzetu kumbe wana symbols
(alama) zao kwa hiyo hawa wakalimani wetu pia wamefundishwa jinsi ya
kufahamu symbols.
"Hata
sisi kwenye haya mashindano wenzetu Watanzania tumewasaidia kujua, kwa
hiyo serikali inaendelea kuwasaidia na kuweka mazingira mazuri kwa
wenzetu viziwi wote na wengine wenye changamoto tutaenzi vipaji vyao ili
waendelee kuonesha vipaji vyao na maandalizi yote hapa yametimia.
"Kwa
niaba ya Serikali ya Tanzania niwashukuru MMDI (Miss & Mister Deaf
International, Inc) kwa kuiamini Tanzania na kuleta mashindano haya hapa
Tanzania," amesema Dkt.Abbas.
Rais Leek
Kwa
upande wake Rais wa Mashindano ya Urembo na Utanashati kwa Viziwi
Duniani (MMDI),Bi.Bonita Ann Leek amesema, miongoni mwa sababu
zilizowashawishi kuyaleta mashindano hayo hapa Tanzania ni pamoja na
ukarimu, upendo na umoja wa Watanzania.
Pia
amesema, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejitengenezea heshima ya
kipekee katika uso wa Dunia kutokana na namna ambavyo inajali utu, amani
na utulivu. "Hivyo ni vigezo muhimu sana na kwa kweli hayo yote
tumeyashuhudia hapa, asanteni sana Watanzania,"amesema Rais Leek.
Mrope
Naye
Rais wa Mashindano ya Urembo, Utanashati na Mitindo kwa Viziwi Afrika
(MMDAF),Habibu Mrope amesema kuwa,maandalizi ya mashindano hayo ambayo
yanatarajiwa kufanyika kesho jijini Dar es Salaam yamekamilika.
"Tuna
mahusiano mazuri sana na Serikali yetu chini ya uongozi wa Rais Samia
na Serikali imetujengea mahusiano mazuri kupitia Rais Samia Hassan.
"Serikali
ndio chombo chenye nguvu kimeendelea kutusapoti sisi walemavu mpaka
hapa tumefikia ametupa heshima kubwa pamoja na Wizara ya Utamaduni,
Sanaa na Michezo. Kila kitu tukiomba anakubali, kila jambo linakwenda,
tunasema asante sana Mheshimiwa Rais Samia kwa kutupa nafasi hii na
kukubali jambo hili lifanyike hapa nchini. Pia tunamshukuru Mheshimiwa
Waziri Mchengerwa kwa ushirikiano wake amebeba dhamana kuongoza hii
wizara.
"Tunawakaribisha
hapa Tanzania nchi yenye amani hapa ni nyumbani, tunawashukuru sana
vile vile ninamshukuru Mheshimiwa Abbas, Katibu Mkuu kwa ushirikiano huu
mzuri na pia Mheshimiwa Mkurugenzi Ishengoma (Dkt.Emanuel Ishengoma)
tumekuwa tukiwasiliana hata usiku, nawashukuru maofisa wa Wizara ya
Utamaduni na Michezo na vyombo vyote vya habari kwa ushirikiano
wenu,"amesema Mrope.
0 Comments