MAKAMU
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema
diplomasia ya nje inahitaji kutumika vyema ili kujenga uelewa, kwa ajili
ya kufungua fursa zaidi za maendeleo ya nchi na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa
Othman ameyasema hayo leo, akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dokta Stergomena Tax, aliyefika Ofisini
kwake Migombani Jijini Zanzibar, kwa lengo la kujitambulisha na
kubadilishana mawazo juu ya mambo mbali mbali ya kazi na maendeleo.
Amesema
kuwa diplomasia ni njia muhimu na inayoweza kutumika kuibua fursa
zinanazopatikana katika Jamii ya Kimataifa na Nchi za Kigeni, pindipo
itatumika vyema katika kujenga uelewa kwa watu, taasisi na hata
Serikali, ili kufanikisha njia mbali mbali za kujiletea maendeleo, bali
kwa Tanzania na hata Mataifa mengine Barani Afrika, huenda hawajaitumia
vyema nafasi hiyo.
Mheshimiwa
Othman ameeleza kuwa kukosekana kwa uelewa huo kunapelekea ukosefu wa
ufuatiliaji wa matukio muhimu yanayojiri ulimwenguni, ambayo kimantiki
ndiyo ambayo yangeliweza kupelekea upatikanaji wa fursa za maendeleo
kupitia taasisi mbali mbali za Kikanda na Kimataifa.
Ametolea
mfano fursa zinazopatikana kupitia Jumuiya ya Kimataifa ya Haki Miliki
za Kitaalamu (WIPO) ambayo yeye amewahi kuitumikia hapo kabla,
akiwakilisha Mataifa ya Afrika.
Hivyo
ametoa wito kwa Wanadiplomasia kuitumia vyema fursa waliyonayo katika
Taasisi na Mataifa ya Kigeni, kujenga uelewa zaidi, ili kuipatia nafasi
Tanzania katika kuelewa matukio muhimu yanayojiri kila siku duniani,
vivutio, na namna ambavyo ulimwengu unakwenda.
Naye
Waziri Tax, amesema kuwa yupo tayari kwaajili ya kazi ya kuitumikia
Nchi katika kujenga uelewa kupitia diplomasia, sambamba na kuhakikisha
ushirikishwaji wa Zanzibar juu ya Mambo ya Muungano, sambamba na fursa
mbali mbali, zikiwemo za Maazimio yanayopitishwa mbele ya Jamii na
Jumuiya za Kimataifa.
Waziri
huyo ambaye ameteuliwa kushika wadhifa huo kupitia hatua ya hivi
karibuni ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia
Suluhu Hassan, kulifanyia mabadiliko madogo Baraza lake la Mawaziri,
ameahidi kutekeleza na kuyafanyia-kazi maagizo na miongozo yote, katika
kuhakikisha Taifa linafaidika kupitia diplomasia ya nje.
0 Comments