NA PETER STEPHEN
MABINGWA
watetezi wa Kombe la Ligi Kuu ya Netiboli Tanzania, TAMISEMI Queens
imeendeleza wimbi lake la ushindi baada jana kuichapa bila huruma timu
ya Mafunzo kutoka Zanzibar, katika michuano inayoendelea katika uwanja
wa Jamhuri mjini Morogoro.
Mchezaji
wa kati wa Mafunzo Zuwena Nassor akijiandaa kurusha mpira kuelekea
goli la Tamisemi huku akizongwa na mchezaji Mecklina Lucas (aliyeruka
juu) wa Tamisemi Queens katika mchezo uliomalizika kwa Tamisemi kuifunga
Mafunzo magoli 40-35.
TAMISEMI
Queens ikijivunia mastaa wake watano wanaochezea timu ya Taifa ya
netiboli walianza mchezo huo kwa kasi ya aina yake, na kuwalazimu
wachezaji wa Mafunzo kuikabili vilivyo kasi ya Tamisemi iliyokuwa
ikiongozwa na mfungaji wao hatari, Lilian Jovin.
Kutokana
na kasi ya mchezo huo, waamuzi walilazimika kupuliza filimbi mara kwa
mara kutokana na faulo walizokuwa wakichezeana wachezaji wa pande zote
mbili.
Hadi
robo ya tatu ya mchezo huo timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu
lakini walikuwa ni Mastaa wa Tamisemi Queens waliobadili mwelekeo wa
mchezo huo katika robo ya mwisho kufuatia uimara wa beki wake mahiri
(GD) Mersiana Samwel ambaye alikuwa akizuia hatari zote kutoka kwa
wachezaji Adela Miraji (GS) na Mainda Rodgers (GA) wa Mafunzo ambao
walikuwa wakilisakama goli la Tamisemi kama nyuki.
Huu
ni mchezo wanne kwa TAMISEMI Queens kushinda mechi zake mfululizo, na
hivyo kuendelea kujisafishia njia ya kulitetea vema kombe lake la Ligi
kuu ya Netiboli Tanzania.
Mchezaji
wa pembeni wa timu ya Mafunzo ya Zanzibar Jane Josephat ‘aliye na
mpira’ akitafuta mbinu ya kuwatoka wachezaji wa TAMISEMI Queens Mersiana
Samwel (GD) kushoto aliyevaa jezi nyeusi na Sophia Komba (WA) wakati
wa mchezo mkali na wa kusisimua uliofanyika jana katika uwanja wa
Jamhuri mjini Morogoro ambapo Tamisemi ilishinda mchezo huo magoli
40-35.
Mara
baada ya mchezo kumalizika wachezaji wa TAMISEMI Queens walishangilia
ushindi huo kwa staili ya aina yake baada ya kujikusanya kwa pamoja na
kukata keki maalum iliyoletwa uwanjani hapo kwa ajili ya kusherehekea
siku ya kuzaliwa ya kocha wao Maimuna Rajabu Kitete.
Akizungumza
uwanjani hapo Kocha Maimuna aliwasifu wachezaji wake kwa namna
walivyojituma uwanjani na kuhakikisha timu yake inapata ushindi huo na
pia kupongeza uwezo wa wachezaji wa timu pinzani kwa jinsi wanavyoleta
ushindani dhidi ya timu yake.
“Mashindano
ya mwaka huu yana ushindani wa aina yake kwani kila timu tunayokutana
nayo inaleta upinzani wa hali ya juu, kila timu imejiandaa kuchukua
ubingwa,” amesema.
Mbali
na mchezo huo, matokeo ya michezo mingine iliyochezwa juzi na jana
yanaonyesha timu za Mafunzo na JKU zilitoka sare kwa kufungana magoli
44-44, JKT Mbweni 59-Zimamoto 44, Nyika 59- Chuo Kikuu Kampala 39, KVZ
55- Magereza Tanzania 32.
Mchezaji
Adela Miraji (GS) wa Mafunzo akifunga mojawapo ya magoli yake dhidi ya
TAMISEMI Queens katika mchezo uliofanyika jana katika uwanja wa Jamhuri
mjini Morogoro ambapo Tamisemi ilishinda mchezo huo magoli 40-35.
Kadhalika Zimamoto 38-KVZ 49, JKU 46-Nyika 51, Magereza Tanzania 41-JKT Mbweni 45 na Chuo Kikuu Kampala 49-Warriors 36.
Michezo
minne inatarajiwa kupigwa leo katika mwendelezo wa mashindano ya Ligi
Kuu ya Netiboli Tanzania ukiwemo mchezo mkali na wa kusisimua kati ya
Tamisemi dhidi ya Nyika Queens kutoka mkoa wa Pwani.
0 Comments