Ticker

6/recent/ticker-posts

IDADI YA WAGONJWA YAONGEZEKA MLOGANZILA .


Idadi ya wagonjwa wanaofika kupata huduma ya matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila imeongezeka kutokana na uboreshwaji wa huduma ikiwemo kuhamishwa kwa Kliniki ya Magonjwa ya Moyo na Kliniki ya Mishipa ya Fahamu kutoka Muhimbili Upanga ambapo kwa sasa wataalamu wanapatikana muda wote Mloganzila.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya utoaji huduma katika Hospitali ya Mloganzila .

Prof. Janabi amesema pamoja kuhamia kwa kliniki hizo kutoka Muhimbili Upanga lakini Kliniki za Magonjwa ya Ngozi, Upasuaji, Usingizi na ganzi, Masikio, Pua na Koo zinaendelea kama kawaida na wataalamu wapo muda wote.

"Pamoja na kliniki hizo, pia kuanzia tarehe 1 Desemba Kliniki ya Magonjwa ya Sukari na Homoni itahamia hapa Mloganzila, wataalamu waliokuwa wanapatikana Upanga wote watapatikana Mloganzila" amesema Prof. Janabi

Ameeleza kwamba ongezeko hilo limekuja na changamoto ya usafiri, Magari yanayokuja Mloganzila kutoka sehemu mbalimbali yameanza kulemewa hivyo ametoa wito kwa wakala wa usafiri wa mabasi yaendayo kasi DART kuongeza idadi ya magari yanayofika Mloganzila ili kurahisisha huduma za usafiri.

Naye Bi. Marietha John ambaye ni ndugu wa mgonjwa anayehudhuria Kliniki ya Mishipa ya Fahamu ameshukuru uongozi wa MNH kwa kuhakikisha wataalamu wanapatikana muda wote na wagonjwa wanapata huduma kwa wakati.

"Mama yangu ana tatizo la kiharusi, anahudhuria hapa kliniki , kwa kweli nashukuru tunapata huduma nzuri na Mama anapata eneo kubwa na lenye utulivu la kufanyia mazoezi" ameeleza Bi. Marietha

Post a Comment

0 Comments