Ticker

6/recent/ticker-posts

TBS WANENA NA WAFANYABIASHARA KATIKA ZIARA YA WAANDISHI WA HABARI TBS JIJINI DAR ES SALAAM

Mkaguzi kutoka kitengo cha Bidhaa zinazotoka nje ya nchi (TBS), Bw. Andalalisye Mwakyonde akizungumza na waandishi wa habari ambao wamefanya ziara katika Makao Makuu ya TBS Ubungo leo Jijini Dar es Salaam. Afisa Usalama wa Chakula Mkuu TBS, Bi. Coletha Sarimbo akizungumza na waandishi wa habari ambao wamefanya ziara katika Makao Makuu ya TBS Ubungo leo Jijini Dar es Salaam.

*********************

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Wazalishaji na waingizaji wa bidhaa wametakiwa kushirikiana na taasisi za serikali ikiwemo Shirika la Viwango Tanzania (TBS) katika kuhakikisha kuwa ubora wa bidhaa zinazozalishwa na kuingizwa nchini unazingatiwa ili kusaidia katika kulinda uchumi wa nchi na kupunguza hasara kwa wafanyabiashara.

Ameyasema hayo leo Novemba 25,2022 Jijini Dar es Salaam, Mkaguzi kutoka kitengo cha Bidhaa zinazotoka nje ya nchi (TBS), Bw. Andalalisye Mwakyonde wakati akizungumza na waandishi wa habari ambao wamefanya ziara katika Makao Makuu ya TBS Ubungo Jijini Dar es Salaam.

Amesema TBS inafanya ukaguzi mipakani na Bandarini ili kuhakikisha kuwa bidhaa zote zinakidhi usalama na ubora uliowekwa hivyo amewataka waingizaji wa bidhaa kufuata taratibu zote pindi wanapotaka kuingiza bidhaa nchini.

"Shirika la Viwango Tanzania lina kampuni tano zinazofanya ukaguzikatika maeneo ya uzalishaji mkubwa wa bidhaa zinazoingizwa nchini ikiwa ni pamoja na CCIC Intertek , Bureau Veritas, SGS pamoja na TUV walioanza shughuli za ukaguzi mapema Agosti mwaka huu". Amesema

Kwa upande wake Afisa Usalama wa Chakula Mkuu TBS, Bi. Coletha Sarimbo amesisitiza umuhimu wa usajili wa bidhaa hususani za chakula na vipodozi katika kuhakikisha ubora na usalama wa bidhaa husika ili kulinda afya za watumiaji na vilevile kusaidia wananchi kupata taarifa sahihi ya bidhaa kulingana na viambata vilivyopo kwenye bidhaa hizo.

Bi.Sarimbo alitoa wito kwa wafanyabiashara wanaoandaa matangazo yanayohusu vyakula na vipodozi kuyawasilisha TBS kwa ajili ya mapitio na baadae kupewa kibali ili kuhakikisha matangazo hayo hayamrubuni mlaji.

Post a Comment

0 Comments