Mkurugenzi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samuel Gwamaka akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 15,2022 Jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samuel Gwamaka akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 15,2022 Jijini Dar es Salaam Mwakilishi wa Mgodi wa Williamson Diamond Bi. Silvia Mulogo akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 15,2022 katika ofisi za NEMC Jijini Dar es Salaam.
***********************
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limewapiga faini ya shilingi bilioni moja Wamiliki wa Mgodi wa Williamson Diamond uliopo Mwadui mkoani Shinyanga kwa kosa la uharibifu wa mazingira katika bwawa la Matope la Mgodi huo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 15,2022 katika Ofisi za NEMC Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samuel Gwamaka amewataka wamiliki wa mgodi huo kulipa faini hiyo ndani ya muda wa siku thelathini kuanzia leo na amewaagiza kuandaa mpango kazi wa kurejesha mazingira katika hali yake ya awali.
“Kwa Sheria na Mamlaka ambayo Baraza tumepewa, tunawaadhibu wamiliki wa mgodi wa Williamson Diamond kiasi cha fedha za kitanzania shilingi Bilioni moja (1 Billion) fedha hiyo ilipwe ndani ya muda wa siku thelathini, pia ndani ya muda huo walete mpango kazi wa kurejesha mazingira katika hali ya awali na ujenzi wa bwawa jipya la kisasa likiwa na vibali vyote kutoka mamlaka husika.” Amesema Dkt.Gwamaka.
Aidha Dkt.Gwamaka amewasisitiza wamiliki wa migodi wote nchini kuhakikisha wanachukua hatua za kitalamu kuhakikisha kwamba mabwawa ya tope katika migodi ya yanajengwa kwa usanifu mkubwa ili kudhibiti athari za kimazingira zinazoweza kujitokeza.
Hata hivyo amesema adhabu hiyo iwe fundisho kwa kampuni nyingine za migodi kuhakikisha kuwa wanaweka miundombinu thabiti na yenye uwezo wa kutumika bila kuathiri mazingira ya eneo husika na watu wake.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mgodi wa Williamson Diamond Bi. Silvia Mulogo amesema wamepokea ripoti ukaguzi kutoka NEMC na kuahidi kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na wataalamu ikiwa ni pamoja na kulipa faini iliyoainishwa kisheria.
“Kwa niaba ya Mgodi, tumeipokea ripoti ya ukaguzi wa bwawa la tope lililopasuka katika mgodi wa Williamson Diamond kutoka NEMC, tutaipitia na kuitolea ufafanuzi pale inapobidi. Tunaahidi kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na wataalamu ili kuweza kudhibiti tatizo hili lisiweze kujitokeza tena kwa mara nyingine.” Amesema Bi.Silvia.
0 Comments