Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Kisekta ambaye pia ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) akisoma maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusu migogoro wa ardhi Mkoani Kagera katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la Shule ya Msingi Rutoro, Wilayani Muleba Mkoani Kagera.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Ridhiwani Kikwete (Mb) akiwaasa wananchi kuheshimu sheria za ardhi katika mkutano wa hadhara kuhusu maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusu migogoro wa ardhi Mkoani Kagera uliofanyika katika eneo la Shule ya Msingi Rutoro, Wilayani Muleba Mkoani Kagera.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) akiwahimiza wananchi kuanzisha miradi ya upandaji miti na ufugaji nyuki katika maeneo watakayokabidhiwa na Serikali wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la Shule ya Msingi Rutoro, Wilayani Muleba Mkoani Kagera.
Baadhi ya wananchi wakimsikiliza Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Kisekta ambaye pia ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) (hayupo pichani) alipokuwa akisoma maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusu migogoro wa ardhi Mkoani Kagera katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la Shule ya Msingi Rutoro, Wilayani Muleba Mkoani Kagera.
Kamati ya Mawaziri wa Kisekta ikiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Kisekta ambaye pia ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) (kulia) ikiwasili katika Kata ya Rutoro Wilaya ya Muleba Mkoani Kagera kwa ajili ya kutoa maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusu migogoro wa ardhi Mkoani humo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Kisekta ambaye pia ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) (kushoto), Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Ridhiwani Kikwete (Mb) (katikati) na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) (kulia) wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Albert Chalamila (hayupo pichani) wakati wa mkutano wa hadhara kuhusu utatuzi wa migogoro wa ardhi Mkoani Kagera uliofanyika eneo la Shule ya Msingi Rutoro, Wilayani Muleba Mkoani Kagera.
Kamati ya Mawaziri wa Kisekta ikiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Kisekta ambaye pia ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) (wa tatu kushoto) katika mkutano wa hadhara kuhusu utatuzi wa migogoro ya ardhi Mkoani Kagera uliofanyika kwenye Kata ya Rutoro Wilaya ya Muleba Mkoani Kagera. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Albert Chalamila.
****************
Serikali imemega baadhi ya maeneo ya Ranchi ya Kagoma yenye ukubwa wa hekta 50,690 na kuyarasimisha kwa wananchi wa Kata ya Rutoro wilayani Muleba mkoani Kagera ili kwa ajili ya shughuli za makazi, kilimo na ufugaji .
Kauli hiyo imetolewa leo na Kamati ya Mawaziri wa Kisekta katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la Shule ya Msingi Rutoro, Muleba .
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) amesema maeneo hayo yatamegwa na kupewa wananchi kwa kuzingatia ushauri wa watalaam.
“Maeneo yatakayomegwa kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu kutoka kwenye ranchi yatawekewa utaratibu wa usimamizi na uongozi wa mkoa ukishirikiana na wilaya ili msigombanie au kufanya jambo lolote ndani ya maeneo hayo” Mhe. Ndaki amesisitiza.
Mhe. Ndaki amewaonya viongozi wa vijiji na vitongoji kuacha tabia ya kugawa maeneo hayo kwa kuwa hawana mamlaka ya kugawa maeneo.
Katika hatua nyingine, amesema Serikali imeridhia kukiacha Kitongoji cha Rwamisha B ambacho kiko wilaya ya Karagwe chenye kaya 480 ambacho awali kiliamuliwa kiondoke.
Mhe. Ndaki ameelekeza mkoa wa Kagera kuandaa mpango wa utekelezaji wa maamuzi ya Kamati ya Mawaziri ya Kisekta yaliyofikiwa ikiwa ni pamoja na kurekebisha mipaka ya vijiji kwa kuzingatia maoni ya wataalamu.
Sambamba na hilo Waziri Ndaki amewatoa hofu wawekezaji walioko katika Ranchi ya Kagoma akiwaeleza kuwa wako salama na Serikali imefanya mazungumzo na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) ili uwekwe utaratibu mzuri ambao utawawezesha kupewa maeneo yatakayomegwa.
Amewaasa wananchi kuwa watulivu wakati wa utekelezaji wa maamuzi ya kamati hiyo na kuacha kuvamia maeneo ili kurahisisha utekelezaji wa maamuzi hayo.
Naye, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Ridhiwani Kikwete (Mb) amewataka wananchi kuendelea kuheshimu sheria za ardhi hususani katika mpango wa maendeleo ya ardhi na kwamba kuna kazi ya kufanya katika kuhakikisha miundombinu na majengo ya eneo la Rutoro yanakaa sawa.
Ametoa rai wananchi hao kuwa watulivu mpaka wataalamu wa ardhi watakapokuja kutoa utaratibu wa maeneo yaliyoachiwa kwa wananchi.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amewataka wananchi wa Kata ya Rutoro kuitumia ardhi waliyoachiwa kwa maendeleo kwa kuanzisha miradi ya upandaji miti pamoja na ufugaji nyuki.
“Nendeni mkapande miti kibiashara mtapata mbao na wakati huohuo mnaweza kuanzisha miradi ya ufugaji nyuki.
Ametoa wito kwa wananchi kutoyavamia maeneo yatakayoachwa kwa Serikali kwa kuwa ni maeneo yanayotunzwa kwa faida ya kizazi cha leo na kinachokuja.
Kamati ya Mawaziri wa Kisekta imehitimisha ziara yake mkoani Kagera na itaendelea na zoezi hilo katika mkoa wa Ruvuma.
0 Comments