Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mary Masanja (Mb), wakiwasili katika Kijiji cha Msai kata ya Mtowa, Wilaya ya Iramba mkoani Singida, kuzungumza na wananchi kwa ajili ya kutatua mgogoro wa mipaka baina ya wananchi wa eneo hilo na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wanaosimamia Hifadhi ya Msitu wa Bonde la Wengere.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akisalimiana na wananchi wa Kijiji Msai kata ya Mtowa, tarafa ya Shelui, Wilayani Iramba mkoani Singida, walipowasili na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mary Masanja (Mb) (hayupo pichani), kwa ajili ya kutatua mgogoro wa mipaka baina ya wananchi wa eneo hilo na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), wanaosimamia Hifadhi ya Bonde la Wembere.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akizungumza na wananchi wa kijiji cha Msai Kata ya Mtowa kuhusu namna Serikali ilivyodhamiria kutatua mgogoro wa mipaka baina ya wananchi na Hifadhi ya Bonde la Wembere, akiwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mary Masanja (Mb) (hayupo pichani).
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiteta jambo na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mary Masanja (Mb), (kushoto), walipotembelea na kukagua eneo la Hifadhi ya Bonde la Wembere, lenye mgogoro baina ya wananchi na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wanaosimamia Hifadhi ya Msitu huo kuhusu mipaka.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (mwenye skafu shingoni), akiambatana na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mary Masanja (Mb) (wa tatu kulia) wakiwasili katika Kijiji cha Ujungu kata ya Mtekente Wilayani Iramba mkoani Singida, kukagua miundombinu ya Wakala wa Huduma ya Hifadhi ya Misitu Tanzania (TFS), iliyoharibiwa na wananchi wa Kijiji hicho kwa madai ya kupinga mipaka mipya iliyowekwa na Wakala wa Huduma za Misitu (TSF) katika maeneo wanayoishi.
Mkuu wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida, Bw. Suleiman Yusuph Mwenda, akiwaonesha kitu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mary Masanja (Mb) hayupo pichani) walipotembelea Hifadhi ya Bonde la Wembere katika Kata ya Mtekente, Wilaya ya Iramba mkoani Singida, kutatua mgogoro wa mipaka baina ya wananchi wa eneo hilo na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wanaosimamia Hifadhi ya Bonde hilo.
Wakazi wa Kijiji cha Msai Kata ya Mtowa, Tarafa ya Shelui Wilaya ya Iramba mkoani Singida, wakifuatilia mkutano wa hadhara ulioitishwa kwa ajili ya kutatua mgogoro wa mipaka baina ya wananchi na Hifadhi ya Bonde la Wembere inayosimamiwa na ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS). Mkutano huo uliwashirikisha Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mary Masanja (Mb) na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Iramba, viongozi wa TFS na wataalam wa masuala ya ardhi kutoka Mkoa wa Singida.
Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WFM, Singida)
*******************
Na Benny Mwaipaja, Singida
SERIKALI imeunda kamati ya kutanzua mgogoro wa mipaka ya ardhi baina ya wananchi na Msitu wa Hifadhi ya Bonde la Wembere unaosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Wilayani Iramba mkoani Singida, uliodumu kwa muda wa miaka mitatu.
Hatua hiyo imechukuliwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Mary Masanja, alipotembelea eneo hilo lenye mgogoro, akiambatana na Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi.
Ziara ya Mawaziri hao wawili katika Hifadhi ya Msitu wa Bonde la Wembere yenye ukubwa wa zaidi ya hekta za mraba elfu 54, unafuatia malalamiko ya wakazi wa eneo hilo ambao wamezuiwa kufanya shughuli zozote za kuwawezesha kujikimu kimaisha kwa vile wako ndani ya hifadhi.
Mheshimiwa Masanja alisema kuwa Serikali inataka kuona mgogoro huo unamalizika na kuitaka kamati hiyo iliyoundwakushughulikia mgogoro huo inakamilisha kazi hiyo kwa wakati kwa kuzishirikisha kikamilifu pande zote zinazohusika ili kupata suluhu ya kudumu.
Pamoja na mambo mengine, kamati hiyo imepewa jukumu la kupitia upya mipaka iliyowekwa na TSF na kulalamikiwa na wananchi wanaoendesha shughuli zao mbalimbali za kiuchumi katika eneo hilo zikiwemo shughuli za uvuvi, kilimo na ufugaji.
Aidha, Mheshimiwa Mary Masanja, aliuagiza uongozi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika Wilaya hiyo ya Iramba, kuwarejeshea wananchi mali zao walizozikamata na kuzishikilia ikiwemo, pikipiki na majembe ili kuendeleza hali ya utulivu na amani iliyopo katika eneo hilo.
Hata hivyo, Naibu Waziri huyo wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Mary Masanja, alikemea kitendo cha baadhi ya wananchi walioharibu miundombinu ya Mradi wa uoteshaji wa kitalu chkijiji cha Ujungu kata ya Mtekente, ikiwemo kuvunja uzio na kuharibu kisima cha maji na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya shilingi milioni 50.
Kwa upande wake Waziri wa Fedha na Mipango, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, alisema hatua iliychukuliwa na Serikali ya kutatua mgogoro huo kwa kuunda kamati ya kupitia upya mipaka inayolalamikiwa na wananchi imekuja wakati muafaka.
Alishauri kamati husika ifanyekazi hiyo kwa weledi na kwa haraka ili mgogoro huo uishe na kuwawezesha wananchi kuendelea na shughuli zao bila hofu lakini pia kuimarisha uhifadhi wa eneo hilo lenye ardhi oevu la Bonde la Wembere.
Aliwataka wananchi hao waendelee kuwa watulivu wakati Serikali inashughulikia mgogoro huo kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi na kwamba anatarajia mgogoro huo utamalizika lakini pia watambue umuhimu wa uwepo wa hifadhi hiyo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadae.
Mgogoro wa ardhi (mipaka) baina ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na wananchi katika Wilaya ya Iramba Mkoani Singida unahusisha wakazi wa kata sita za Urughu, Mketenke, Mtowa, Mgongo, Ntwike, Tulya na Kadaru.
0 Comments