SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limemaliza kampeni yake ya kutoa elimu kwa umma katika wilaya za Iramba, Mkalama, Ikungi na Halmashauri ya Wilaya ya Singida mkoani Singida kuhusiana na umuhimu wa kusoma taarifa zilizopo katika bidhaa na kununua bidhaa zilizothibitishwa na shirika hilo.
Aidha, kampeni hiyo ilienda sambamba na kuwahamasisha wajasiriamali wadogo kuthibitisha ubora wa bidhaa zao na wafanyabiashara kutakiwa kusajili maduka ya chakula na vipodozi iliwafikia wananchi 6,800.
Kampeni hiyo iliyoanza Novemba 28, mwaka huu ilihitimishwa jana ambapo ilikuwa ikifanyika katika maeneo mbalimbali yenye mikusanyiko ya watu wengi ikiwemo sokoni, stendi, minadani na maeneo mengine ya wazi ambapo wananchi walijitokeza kupata elimu na ufahamu wa masuala mbalimbali yahusuyo Ubora wa bidhaa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Iramba, Michael Matomora, aliipongeza TBS kwa kutoa elimu kwa wananchi na alishauri kufanya kaguzi za kushtukiza mara kwa mara madukani hususani katika bidhaa za ujenzi kama nondo na mabati.
Kwa upande wake Mkaguzi wa TBS, Magesa Mwizarubi aliwakumbusha wananchi kutambua kuwa vita ya bidhaa hafifu sio ya shirika hilo pekee yake, bali ni ya Taifa kwa ujumla.
Magesa aliwafafanulia wananchi umuhimu wa viwango katika maisha yao ya kila siku na vile vile kuwafahamisha fursa ya huduma ya kuthibitisha ubora wa bidhaa bure zinazozalishwa wajasiriamali wadogo.
Hata hivyo, aliwataka wawe mabalozi kwa kuhamasisha umuhimu wa matumizi ya bidhaa zenye ubora katika jamii wanazoishi. Alitoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa pindi pale wanapokutana na bidhaa zilizokwisha muda wake au wanapotilia shaka bidhaa yoyote katika soko.
"Kwa wafanyabiashara ni muhimu kufuatilia taratibu sahihi za usajili wa bidhaa au majengo ya chakula na vipodozi kwa kutembelea ofisi ya TBS iliyopo karibu au kupiga katika kituo cha huduma kupitia mawasiliano yaliyotolewa," alisema.
Kupitia kampeni hiyo shirika limeweza kuwafikia wananchi 6,839 kati yao wajasiriamali wanawake ni 89.
Alifafanua kwamba kampeni hiyo ni endelevu na itaendelea katika wilaya za mkoa wa Mbeya.
0 Comments