**********************
Na Mbaraka Kambona, Pwani
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amesema kuwa Wizara yake imeanzisha vituo atamizi kuwawezesha vijana kufuga kwa tija ili kujikwamua kimaisha na pia kuwa ni kichocheo kwa wafugaji wengine kujifunza kwa vitendo na kubadilika kutoka katika ufugaji wa kienyeji na kufanya ufugaji wa kisasa utakaowaletea tija zaidi na kupunguza migogoro isiyo ya lazima kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.
Ndaki aliyasema hayo wakati akifunga Mafunzo Rejea kwa Maafisa Ugani wa Kanda ya Mashariki yaliyofanyika mkoani Pwani Disemba 13, 2022.
Alisema kuwa Wizara yake imewekeza na inahamasisha Vijana kushiriki katika uzalishaji wa mifugo kupitia Vituo Atamizi ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 vijana 240 waliohitimu vyuo vya Mafunzo ya Mifugo wamedahiliwa na kuanza mafunzo ya unenepeshaji wa ng’ombe katika vituo nane (8).
“Kwa mantiki hiyo nawahimiza wadau mbalimbali kuwekeza na kuhamasisha vijana kujiunga na Vituo atamizi ambavyo vimeanzishwa na Wizara kwa sababu vijana hao wakimaliza mafunzo hayo watasaidia wafugaji wengine kubadilika na kuanza kufuga kwa tija,” alisema Ndaki
Aliongeza kwa kusema kuwa wanatarajia kuwa utaratibu huo wa vituo atamizi utaendelea kwa sababu wanaamini kupitia vituo hivyo ni njia nzuri ya kuwafikia vijana, kutoa ajira kwa vijana lakini pia itasaidia wafugaji wajifunze kwa vitendo ufugaji wa kisasa na kuachana na ufugaji wa kienyeji.
“Mwakani tunatarajia kuwa na vijana wengi zaidi kwa sababu tutaongeza bajeti kuhusu vituo hivi ili tuweze kuwachukua vijana wengi zaidi hata kufikia 1000, kwa sababu vijana hawa wakitawanyika kote nchini wataleta mageuzi kwenye ufugaji wetu,”alifafanua
Aidha, alisema kuwa huduma za ugani ni kiungo muhimu kati ya watafiti na wafugaji ili kupata ufugaji wenye tija hivyo ni vyema maafisa ugani wakaimarisha mahusiano mazuri ili waweze kufikia malengo tarajiwa.
“Nitoe rai kwenu kujenga ushirikiano madhubuti baina yenu na wafugaji utakaowezesha kutoa taarifa sahihi, kusambaza teknolojia, kuelimisha, kutoa ushauri wa kitaalamu na kupata mrejesho,”alisema
Waziri Ndaki alisema kuwa wanatambua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya mifugo hususan katika utoaji wa huduma za Ugani hapa nchini lakini tayari Wizara kupitia Mpango wa Mabadiliko wa Sekta ya Mifugo imebainisha mikakati na afua mbalimbali za kuzipatia suluhisho changamoto hizo.
“Miongoni mwa juhudi za serikali ni pamoja na kuanza kutoa Mafunzo Rejea kwa Maafisa Ugani Watakaowafundisha Wengine (Trainer of Trainee) ambapo jumla ya Maafisa Ugani 800 watafikiwa kwa mwaka wa fedha, 2022/2023. Aidha, Wizara inatarajia kutoa mafunzo elekezi kwa wafugaji 182,200 nchini ambapo ninyi mtatusaidia sana katika kutekeleza jukumu hilo,”alifafanua
Aliongeza kuwa katika kutatua changamoto ya ukosefu wa vitendea kazi vya kutolea huduma za Ugani, Wizara imepanga kununua pikipiki 1,200 ambazo zitaongeza chachu kama vitendea kazi muhimu katika Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Vilevile Wizara imeanza matumizi ya mifumo ya TEHAMA (M-Kilimo na Digital Agricultural Service Portfolio (Ugani Kiganjani) kwa lengo la kuwafikia wafugaji wengi na kutoa mrejesho wa kila kazi ambayo Afisa Ugani atakuwa ametekeleza katika eneo lake.
0 Comments