Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akifafanua jambo kwa waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Jengo la Mkapa. Mhe. Senyamule ametangaza Kampeni Maalumu ya upandaji miti katika Mkoa wa Dodoma kwa lengo la kuikijanisha Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akitoa maelezo kwa wandishi wa habari juu ya kampeni ya upandaji miti katika Mkoa wa Dodoma.
**************************
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na wadau wa mazingira, leo tarehe 30 Desemba 2022, imetangaza kampeni maalumu ya upandaji miti katika Mkoa wa Dodoma lengo hasa likiwa ni kutimiza lengo la kampeni ya kuikijani Dodoma.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule alipokua akizungumza na waandishi wa Habari kwenye ukumbi uliopo kwenye jengo la Mkapa, ofisini kwake.
“Sote tunafahamu kuwa msimu wa mvua umeanza hivyo, ni wakati sahihi kwa wananchi na wakazi wote wa Dodoma kutekeleza kwa vitendo Kampeni ya upandaji miti kuanzia ngazi ya Kaya, Kata, Vijiji, Vitongoji hadi ngazi ya Taasisi na msisitizo wa mwaka huu ni kwamba miti yote itakayopandwa hakikisheni inakua na kustawi vizuri” Amesisitiza Mhe. Senyamule
Kadhalika, Mkuu wa Mkoa amezitaja baadhi ya faida za uwepo wa miti ya kutosha katika mazingira yetu na Mkoa kwa ujumla kuwa ina mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi na jamii kwa ujumla kwani misitu inatoa asilimia 45 ya malighafi za ujenzi, hunyonya hewa ukaa, hutupatia hewa safi, kulinda na kuhifadhi vyanzo vya maji na pia huchangia ongezeko la pato la Taifa.
“Ninafahamu wenzetu wakala wa misitu TFS wamezalisha miche ya miti ya kutosha pale katika kitalu cha miti eneo la Mailimbili na miche hiiinagawiwa bure, hivyo natoa rai kwa wanadodoma kufika pale kuchukua miche ya miti na kupanda katika maeneo yenu. Tutapita kukagua kila nyumba na kuona miti mitano iliyopandwa na wale wasiopanda watachukuliwa hatua kwa kuwa hii ni sehemu yasheria ndogo tulizonazo kwenye Halmashauri” Ameongeza Mh. Senyamule
Kampeni ya upandaji miti Mkoa wa Dodoma inayotarajiwa kuanza Desema 31hadi msimu wa mvua utakapokwisha, imelenga Halmashauri zote nane za Mkoa kwani lengo kuu la Mkoa ni kila Halmashauri kupanda miti 1,500,000 kwa mwaka licha ya baadhi ya maeneo kupewa kipaombele kama eneo la Ihumwa kwenye chanzo cha maji cha DUWASA na katika bonde la Mzakwe.
0 Comments