RUVUMA
Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Hamis Kamando amesema kuwa kutokana na uwepo wa wingi wa madini ya makaa ya mawe katika mkoa wa Ruvuma ikiwa ni tani milioni 328, kampuni nyingi za kitanzania zimepata mwamko na kuwekeza hali iliyopelekea ofisi yake kuendelea kufanya vizuri kwenye ukusanyaji wa maduhuli kwa kuvuka malengo ya kila mwaka yanayowekwa na Serikali katika ofisi yake.
Mhandisi Kamando aliyasema hayo mapema jana tarehe 20 Januari, 2023 mkoani Ruvuma kwenye mahojiano maalum ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kipindi maalum chenye lengo la kuangalia mchango wa Sekta ya Madini katika kuwawezesha watanzania kiuchumi pamoja na uboreshaji wa huduma za jamii katika mikoa ya Njombe, Ruvuma na Mtwara.
Akieleza mafanikio ya Sekta ya Madini katika mkoa wa Ruvuma yaliyochangiwa na uwekezaji katika uchimbaji wa makaa ya mawe, Mhandisi Kamando alisema kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021-2022 ofisi yake ilipangiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 12 na kufanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 21 ikiwa ni asilimia 175 ya lengo lililowekwa katika mwaka husika.
Aliendelea kusema kuwa katika mwaka wa fedha 2022-2023 ofisi yake iliwekewa lengo la kukusanya shilingi bilioni 26.3 na kuongeza kuwa kuanzia kipindi cha mwezi Julai mwaka 2022 hadi tarehe 19 Januari, 2023 ofisi imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 23.1 ikiwa ni asilimia 87 ya lengo la mwaka husika na kuendelea kusema kuwa ofisi imejipanga kukusanya hadi shilingi bilioni 35 ifikapo mwezi Juni mwaka huu.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Kamando alieleza kuwa ofisi yake imeendelea kubuni mikakati mbalimbali ya usimamizi wa ukusanyaji wa maduhuli kwa ubunifu wa hali ya juu ambapo inatarajia kuwa miongoni mwa mikoa minne inayoongoza kwenye ukusanyaji wa maduhuli katika Sekta ya Madini.
Alieleza kuwa mafanikio mengine kuwa ni pamoja na kampuni za uchimbaji wa madini ya makaa ya mawe katika mkoa wa Ruvuma kuendelea kushirikisha wananchi kwenye utoaji wa huduma kwenye migodi kupitia kanuni za ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini na uboreshaji wa huduma za jamii.
“Kutokana na elimu ambayo imekuwa inatolewa na Ofisi ya Madini Mkoa wa Ruvuma kwa kampuni za uchimbaji wa makaa ya mawe kuhusu ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini, kampuni zimeanza kutoa zabuni mbalimbali ikiwa ni pamoja na usambazaji wa bidhaa za vyakula na vifaa kwenye migodi hivyo kupelekea wananchi kujipatia kipato huku Serikali ikikusanya kodi mbalimbali,” alisisitiza Mhandisi Kamando.
Katika hatua nyingine, sambamba na kupongeza kazi kubwa inayofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais, Philip Mpango, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko pamoja na uongozi wa Wizara ya Madini kwa kushirikiana na uongozi wa Tume ya Madini kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini, aliwataka wananchi wengi kuchangamkia fursa za uwekezaji katika mkoa wa Ruvuma.
“Sambamba na uwepo wa madini ya makaa ya mawe, yapo madini mengine ya vito mbalimbali vya thamani ikiwa ni pamoja na almasi yanayopatikana katika maeneo tofauti ya mkoa wa Ruvuma, wawekezaji wote wanakaribishwa na milango ya ofisi ipo wazi muda wote kutoa msaada ili wananchi wengi zaidi waweze kunufaika,” alisema Mhandisi Kamando.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wawekezaji waliowekeza katika mkoa huo waliipongeza Serikali kupitia Wizara ya Madini na Tume ya Madini kwa kuweka mazingira ambayo ni rafiki na kuendelea kutatua changamoto mbalimbali kwenye Sekta ya Madini.
Akielezea manufaa ya uchimbaji wa madini ya makaa ya mawe, Mjumbe wa Bodi na Msimamizi wa Mradi wa Kampuni ya Jitegemee Holdings Company Limited inayojihusisha na uchimbaji wa makaa ya mawe katika Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Boscow Mabena, alisema kuwa tangu kuanza kwa shughuli za uzalishaji mwaka 2021 kampuni imefanikiwa kulipa kiasi cha shilingi bilioni 7.01 ikiwa ni kodi, tozo na michango mbalimbali Serikalini.
Aliendelea kutaja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na ajira kwa watumishi wa kada mbalimbali 147, utoaji wa michango mbalimbali kwenye vijiji vinavyozunguka mgodi na kuongeza kuwa kampuni imeshakaa na vijiji kwa ajili mapendekezo ya miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na ujenzi wa zahanati, mabweni katika shule za msingi na sekondari na maji kabla ya utekelezaji wake pamoja na utoaji wa fursa za huduma za vyakula kwenye mgodi.
Alitaja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na kutwaa tuzo mbili kutoka katika mamlaka za Serikali ikiwemo tuzo ya mshindi wa pili ya mchangiaji mkubwa wa tozo za Serikali katika pato la nchi kutoka Wizara ya Madini na tuzo ya pili ikiwa ni ya mshindi wa pili wa mchangiaji mkubwa wa kodi za Serikali katika mkoa wa Ruvuma kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Wakati huohuo, Meneja wa Mgodi wa Ruvuma Coal Limited, Benedict Mushingwe akielezea hali ya uzalishaji wa makaa ya mawe katika mgodi huo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2020 alisema kuwa mgodi umeendelea kufanya vizuri ambapo katika kipindi cha Januari hadi Desemba mwaka 2020 mgodi ulizalisha tani 600,000 na katika kipindi cha Januari hadi Desemba, 2022 mgodi ulizalisha tani milioni 1.9 na kuuza ndani ya nchi na katika nchi za nje kama vile Kenya, Uganda, Rwanda, Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, Senegal, Ghana, Poland, India, Ufaransa, Uholanzi na nchi nyingine za Ulaya.
Alisema kuwa kupitia uzalishaji wa makaa ya mawe kampuni ilifanikiwa kulipa kiasi cha shilingi bilioni 66.8 Serikalini tangu kuanzishwa kwake sambamba na kutoa ajira 785 huku waajiriwa 379 wakiwa wanatoka maeneo ya karibu na mgodi.
Aliendelea kueleza mafanikio mengine kuwa ni pamoja na utoaji wa fursa mbalimbali za utoaji wa huduma kwenye mgodi ambapo wananchi wameunda vikundi na kuanza kutoa huduma za vyakula, ujenzi wa ofisi ya kijiji cha Paradiso, zahanati na kusisitiza kuwa mgodi unajipanga zaidi kuendelea kuboresha maisha ya wananachi wanaoishi katika mgodi pamoja na utunzaji wa mazingira.
0 Comments