Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mekomariro wilayani Bunda mkoani Mara, ambapo amewaeleza wananchi hao kuwa eneo la kituo cha kupumzishia mifugo Buhemba halijauzwa na hakuna mwekezaji yoyote aliyepatiwa eneo hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mhe. Joshua Nasari akiwasalimu wananchi wa Kijiji cha Mekomariro wilayani Bunda mkoani Mara ambapo amewataka kufuata mipango ya matumizi ya ardhi inayowekwa kwenye vijiji ili migogoro isiwepo.
Mbunge wa Jimbo la Bunda Vijijini, Mhe. Boniphace Getere akiwasilisha malalamiko ya wananchi wa Kijiji cha Mekomariro ambapo amesema kuwa wananchi hao wanalalamika kuwa eneo la kituo cha kupumzishia mifugo Buhemba amepewa mwekezaji.
Afisa Mifugo Mkoa wa Mara, Yusuph Kuwaya (wa pili kulia) akimuonyesha Waziri wa Mifugo na Uvuvi eneo la kituo cha kupumzishia mifugo Buhemba wakati alipofanya ziara ya kikazi katika eneo hilo.
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mekomariro wilayani Bunda mkoani Mara wakimsikiliza Waziri wa Mifugo na Uvuvi (hayupo pichani) wakati alipofanya ziara ya kikazi katika Kijiji hicho na kuzungumza na wananchi hao.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akisaini kitabu cha wageni Ofisini kwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda mkoani Mara wakati alipofanya ziara ya kikazi katika wilaya hiyo.
................
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amewahakikishia wananchi wa Kijiji cha Mekomariro kuwa eneo la Kituo cha Kupumzishia Mifugo Buhemba kuwa halijauzwa na hakuna muwekezaji yeyote aliyepatiwa eneo hilo.
Waziri Ndaki ameyasema hayo leo (07.01.2023) wakati alipokuwa kwenye ziara ya kikazi kwenye Wilaya Bunda mkoani Mara ambapo alizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mekomariro waliokuwa wakilalamika kuwa eneo hilo limechukuliwa na mwekezaji.
Waziri Ndaki amewaeleza wananchi hao kuwa eneo hilo halijauzwa na halijatolewa kwa mwekezaji yoyote. Serikali bado inayo mipango ya kulitumia eneo hilo kwa malengo yaliyokusudiwa kwa kutengwa kwake. Hivyo wananchi wametakiwa kuwa watulivu na kutosikiliza maneno yanayozushwa kuhusu matumizi ya eneo hilo kwa kuwa kama serikali itataka kubadilisha matumizi itatangaza.
Kamati ya Mawaziri Nane (8) wa kisekta iliamua kuwa sehemu ya eneo hilo la kituo ligawanywe kwa wananchi kwa kufuata taratibu, na eneo linalobakia liendelee kumilikiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo).
“Kwa kuwa Kamati ya Mawaziri wa Kisekta ilishatoa maelekezo ya kuligawanya eneo, Kijiji cha Mekomariro kimepewa hekta 794.92 na Vijiji vya Mirwa na Magunga vimepatiwa hekta 194.94, hivyo wataalam wanafanya upimaji katika eneo hilo lengo ni kutambua mipaka ya eneo litakalotolewa kwa vijiji hivyo na sio kuwatishia wananchi au kumpatia mwekezaji,” alisema
Waziri Ndaki amewataka wananchi hao kuwa watulivu wakisubiri upimaji unaofanywa kukamilika ili waweze kutambua eneo ambalo wanapatiwa na kuacha kuvamia eneo hilo na kufanya shughuli mbalimbali zikiwemo za ujenzi na kilimo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mhe. Joshua Nasari amewataka wananchi hao kutozalisha migogoro ya ardhi kutokana na kutoheshimu mipango inayowekwa ya matumizi ya ardhi katika Kijiji.
Nasari amesema kuwa lipo eneo lililotengwa kwa ajili ya malisho ya mifugo lakini baadhi ya wanakijiji wanalitumia kwa kujenga makazi na kilimo, hivyo amewataka wote wanao litumia eneo hilo nje ya utaratibu uliowekwa kuacha mara moja na kuondoka kwani hatua zitachukuliwa dhidi yao.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi Boniphace Getere ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Bunda Vijijini amemshukuru Waziri kwa kufika katika Kijiji cha Mekomariro kuona eneo lililo na mgogoro na kuwasikiliza wananchi. Pia amemuomba Mkuu wa Wilaya kuhakikisha eneo hilo lililotengwa kwa ajili ya malisho linasimamiwa na viongozi wa wilaya zote za Bunda, Butiama na Serengeti kwa kuwa eneo hilo lipo ndani ya wilaya hizo.
0 Comments