Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na Wajumbe wa Mkutano wa Baraza Kuu la Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) wakati wa ufunguzi wa mkutano wa baraza hilo uliofanyika jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) ambaye ni Rais wa TUCTA Ndg. Tumaini Nyamhokya akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kufungua Mkutano wa Baraza Kuu la Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania.Baadhi ya Wajumbe wa Mkutano wa Baraza Kuu la Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati akifungua mkutano wa baraza hilo jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa TALGWU Mkoa wa Mara, Dkt. Magreth Shaku akitoa neno la shukrani kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kwa niaba ya wajumbe wa Mkutano wa Baraza Kuu la Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) mara baada ya Waziri huyo kufungua mkutano wa baraza hilo jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe waliohudhuria Mkutano wa Baraza Kuu la Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) mara baada ya Waziri huyo kufungua mkutano wa baraza hilo jijini Dodoma.
*********************
Na. Veronica Mwafisi-Dodoma
Tarehe 17 Januari, 2023
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema Serikali haitosita kuwachukulia hatua waajiri katika taasisi za umma ambao watabainika kushughulikia mashauri ya kinidhamu ya watumishi wa umma bila kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma iliyopo.
Mhe. Jenista amesema hayo jijini Dodoma, wakati akifungua mkutano wa Baraza Kuu la Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU).
Mhe. Jenista amesema, mashauri ya kinidhamu yanachukua muda mrefu bila sababu ya msingi tena kinyume na Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2022 na Sheria ya Utumishi wa Umma Sura ya 298, hivyo kusababisha watumishi ambao wana mashauri ya kinidhamu kutokuwa na tija kiutendaji na kwa wananchi wanaopaswa kuhudumiwa.
Mhe. Jenista amefafanua kuwa, kutokana na waajiri kushughulikia mashauri ya kinidhamu kwa muda mrefu bila sababu za msingi, Serikali inalazimika kuingia gharama za kuendesha mashauri hayo ambayo kama maamuzi yangetolewa kwa wakati, Serikali ingeepukana na gharama hizo.
Mhe. Jenista amesema, shauri la kinidhamu likichukua miaka 3 linamuathiri kiutendaji na kisaikolojia mtumishi atakayekutwa na hatia au kubainika kutokuwa na hatia, hivyo kulisababishia taifa hasara ikiwa ni pamoja na kuwanyima wananchi haki yao ya msingi ya kupata huduma bora.
“Ninawaomba TALGWU pindi mnapoona kuna mienendo ya waajiri isiyoridhisha katika uendeshaji wa mashauri ya kinidhamu, msisite kutupa taarifa ili tuchukue hatua stahiki,” Mhe. Jenista amesisitiza.
Mhe. Jenista ameongeza kuwa, kwa kutambua umuhimu wa rasilimaliwatu katika taifa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipapanga kikamilifu kusimamia Utumishi wa Umma na Utawala Bora nchini.
Akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa Mkutano wa Baraza Kuu la Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU), Mwenyekiti wa TALGWU Mkoa wa Mara, Dkt. Magreth Shaku amesema TALGWU imeanza kufanyia kazi changamoto ya mashauri ya kinidhamu kuendeshwa kwa muda mrefu, kwa kutoa elimu ya haki na wajibu kwa wanachama wake ili wasiathirike kiutendaji na kisaikolojia kutokana na mashauri yao ya kinidhamu kuendeshwa bila kuzingatia taratibu.
Aidha, Dkt. Shaku amehaidi kuwa, TALGWU itaendelea kufanyia kazi changamoto hiyo ya mashauri ya kinidhamu kuendeshwa kwa muda mrefu, ili ifikie lengo lake la kutoa huduma bora kwa wanachama na wananchi kama ambavyo kaulimbiu ya chama inavyosema ‘TALGWU chama imara, huduma bora kwa wanachama’.
0 Comments