Ticker

6/recent/ticker-posts

WAKURUGENZI WA HALMASHAURI WAHIMIZWA KUSIMAMIA MIRADI YA TASAF KIKAMILIFU

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (katikati) akizungumza na Watendaji wa Halmashauri ya Mji Geita na Halmashauri ya Wilaya ya Geita wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Geita.

Sehemu ya Watendaji wa Halmashauri ya Mji Geita na Halmashauri ya Wilaya ya Geita wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (katikati meza kuu) mara baada ya Naibu Waziri huyo kukagua miradi ya TASAF wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Geita.


Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Msangi Tsetonga akifafanua jambo kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri Ndejembi, iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Halmashauri ya Mji Geita na Halmashauri ya Wilaya ya Geita.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (wapili kutoka kulia) akielekea kukagua madarasa ya shule ya Msingi Kivukoni yaliyopo katika Halmashauri ya Mji Geita wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Geita, wengine ni watendaji wa mkoa huo.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (aliyenyanyua mikono) akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Nyanza mara baada ya kukagua madarasa na vyoo vya shule ya Kivukoni vilivyojengwa kwa ufadhili wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) mkoani Geita.


Mwonekano wa darasa lililopo shule ya Msingi Kivukoni katika Halmashauri ya Mji Geita, lililojengwa kwa ufadhili wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

*********************************

Na. Veronica Mwafisi - Geita Tarehe 29 Januari, 2023



Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kusimamia kikamilifu miradi inayotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kama wanavyosimamia miradi mingine ya maendeleo.

Mhe. Ndejembi amewahimiza wakurugenzi hao, wakati akizungumza na Watendaji wa Halmashauri ya Mji Geita na Halmashauri ya Wilaya ya Geita alipokuwa akihitimisha ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma pamoja na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Geita.

Mhe. Ndejembi amehimiza miradi ya TASAF kusimamiwa vizuri kama inavyosimamiwa miradi mingine ya maendeleo kwani miradi yote inatekelezwa na Serikali chini ya uongozi makini wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amedhamiria kuliletea taifa maendeleo.

Mhe. Ndejembi amesema, katika utekelezaji wa miradi ya TASAF inaonyesha kuwa wakurugenzi na watendaji wa halmashauri hawashiriki kikamilifu katika usimamizi na badala yake huwaachia waratibu na watendaji wa TASAF.

“Usimamizi wa miradi ya TASAF unapaswa kupewa kipaumbele, hivyo wakurugenzi ni lazima waisimamie miradi hii kikamilifu kwa sababu fedha inayotumika upatikanaji wake unatokana na jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Mhe. Ndejembi amefafanua kuwa, miradi ya TASAF ikisimamiwa kikamilifu kama ambavyo inavyosimamiwa miradi mingine ikiwemo ya elimu, afya na miundombinu ni dhahiri kuwa, watanzania watanufaika na taifa litapiga hatua katika mendeleo.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mji Geita, Mhe. Joseph Lugaila amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na wasaidizi wake kwa kuwezesha utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo katika Mkoa wa Geita.

Aidha, Mhe. Lugaila amemshukuru Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kwa kufanya ziara ya kikazi katika mkoa wa Geita yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.

Post a Comment

0 Comments