Na OR TAMISEMI
Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa amekagua utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa katika hospitali ya Wilaya Namtumbo ya kuondolewa na kuwekwa milango yenye ubora kulingana na thamani ya fedha katika majengo yanayoendelea kujengwa katika hospitali hiyo.
Waziri Mkuu amekagua utekelezaji wa maelekezo hayo wakati akikagua ujenzi wa hospitali ya Wilaya Namtumbo mkoani Ruvuma, Leo tarehe 06 Januari 2023 ambapo amembatana na Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dkt. Festo J. Dugange (Afya).
Waziri Mkuu alitoa maagizo hayo tarehe 18 Oktoba 2022 wakati wa ziara yake wilayani humo ambapo aliagiza milango 10 iondolewe na kuwekwa mingine yenye viwango ifikapo Januari 4, 2023.
Kufuatia utekelezaji huo, Mheshimiwa Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na utekelezaji wa maelekezo hayo ambapo hadi sasa jumla ya milango 67 kati ya 84 imeondolewa na kuwekwa yenye ubora na milango 15 kati ya 54 imewekwa katika majengo mapya ambayo yalikuwa hayajawekwa milango.
Akizungumza na wananchi wa eneo hilo, Mheshimiwa Majaliwa amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya afya ili kusogeza huduma muhimu za kijamii karibu na wananchi.
Aidha, Waziri Mkuu amewataka wakuu wa Idara katika halmashauri zote nchini kusimamia kikamilifu utekelezaji wa shughuli zote za kimaendeleo katika maeneo yao ili kuhakikisha fedha zinazoletwa na Rais Dkt. Samia kwa ajili ya ujenzi wa miradi zinatumika ipasavyo.
Mpaka sasa hospitali hiyo imepokea shilingi bilioni 4.2 kutoka Serikali kuu ambapo majengo 20 yameshajengwa, majengo 13 yamekamilika, majengo 5 yapo katika hatua za mwisho za ukamilishaji na 2 yapo kwenye hatua za upauaji na upigaji ripu.
0 Comments