*********************
NA MWANDISHI WETU
MTUME na Nabii Shile Mwasha (Nabii wa Rufaa) wa Huduma ya Ufunuo wa Kristo na Kanisa la Miujiza lililopo Bunju Kilimani jijini Dar es Salaam amesema kuwa,mwaka huu anaiona Tanzania mpya chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan huku akisisitiza umuhimu wa maombi kwake na Taifa.
Ameyasema hayo leo Februari 22, 2023 wakati akitangaza mwaka wa Bwana uliokubalika katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam.
"Jambo kubwa ambalo nimekuja nalo leo ni kutangaza mwaka wa Bwana uliokubalika, watu wengi hawajui jina la huu mwaka, lakini Mungu ameniambia niwaambie kuwa, mwaka huu unaitwa mwaka wa moto, kwamba mwaka 2023 ni mwaka wa moto.
"Kwa hiyo kuna maelekezo ambayo Roho mtakatifu amenipa mimi kama Nabii wa Rufaa, unajua manabii wapo wengi, lakini neema ambayo nimepewa mimi Nabii wa Rufaa, kama kuna hospitali ipo ya Rufaa, kama kuna Mahakama ipo ya Rufaa na hata kama kuna manabii wapo wa rufaa,sasa mimi kipengele Mungu alichonipa ni kutangaza mwaka wa Bwana.
"Mwaka ambao mimi ninatangaza katika ulimwengu wa Roho ndiyo ambao una declare-demarcation ambao ni wa rufaa.
"Kwa mwaka huu ambacho ninasema ni kwamba kuna kitu ambacho ninakiona katika ulimwengu wa roho, ninaona Tanzania mpya sana, lakini tunatakiwa kumuombea Mama Samia (Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa sababu ipo neema juu yake, lakini pia tuombe kwa ajili ya watoto wa viongozi na familia mbalimbali maana ninaona wanachanua sana na wakistawi sana na ninaona mafanikio sana kupitia Serikali ya Tanzania na ninaona mafanikio pia kupitia Serikali hii ya CCM.
"Kwa hiyo tumuombee Mama Samia, na pia tumpongeza sana kwa ajili ya kusaidia na kuongeza kwa sababu pia nilitabiri kuhusu mwezi wa Ephata, kwamba utakuwa ni mwezi wa kufunguliwa, na nimpongeza sana Mama Samia kwa kuongeza Boom la Wanafunzi, hongera sana Mama. Hilo ni jambo kubwa sana ambalo amefanya, na ninaona neema kwake mbele, na tuendelee kuomba kwa sababu ipo vita na tutaendelea kuomba na kukemea.
"Kama nilivyosema huu ni mwaka wa moto, na watu wanatakiwa kuingia kwenye moto kwa sababu mwaka wa moto ni mwaka wa majanga, kwa hiyo huu mwaka kwa muda wa miezi minne utakuwa na majanga ya kufuatana, kwa hiyo inawezekana hata kesho ikawa kuna janga.
"Cha msingi ni kwamba upo katika moto wa roho mtakatifu, kwa sababu ambacho kitakusaidia kuokoka katika majanga ni ile moto ya roho mtakatifu. Kama haupo kwenye moto wa roho mtakatifu haya majanga hautayaweza, ndiyo maana kwa mwaka huu jambo pekee ambalo ninawaambia Watanzania wamgeukie Mungu,maana yake Mungu ndiye atawaokoa na huu moto na pia ninaiambia Dunia imgeukie Mungu,na ndiyo maana Mussa alipoona moto alisema,nitageuka ndani ya maono haya.
"Lengo la haya majanga yote ni nini, Mungu anaongea na Dunia, Mungu anaongea na Uturuki,Mungu anaongea na nchi kwamba zimgeukie yeye, zianze kumwangalia yeye ndiyo haya majanga yataisha.Kwa hiyo lengo la Mungu ni watu waokolewe.Lakini haya majanga mwisho wake ni mwezi wa nne, na nimeona katika ulimwengu wa roho kuwa mwezi wa tatu majanga yatakuwa mengi sana,"amefafanua Nabii Mwasha.
Pia amesema, Mungu amemwambia aiombee Jumuiya ya Afrika Mashariki kwani, alimuona mmoja wa marais wa jumuiya hiyo akipunga mkono.
"Katika ulimwengu wa roho nilimuona mmoja wa marais wa Afrika Mashariki akipunga mkono, sitamtaja kwa sasa.Lakini pia roho wa Mungu ameniambia tuombe sana, na tuendelee kuiombea nchi yetu, kwa hiyo mwaka 2023 ni mwaka ambao tunapaswa kukaa katika moto wa roho mtakatifu.Pia katika mwaka huu nimepewa majina mapya 12 ya miezi yaliyobeba unabii wa hatima ya miezi 12,"amefafanua Nabii Mwasha.
0 Comments