Ticker

6/recent/ticker-posts

TANZANIA KUIPA USHIRIKIANO INDIA KUANZISHA CHUO CHA TEKNOLOJIA NCHINI


Serikali ya India inatarajia kuazisha Chuo cha Teknolojia (Indian Institute of Technology) nchini Tanzania ambacho kitakuwa kinatoa kozi ya masuala ya Tehama na kozi nyingine zinazoendana na mlengo huo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam mara baada ya kuongea na timu kutoka Chuo hicho Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda amesema Serikali ya Tanzania itashirikiana na nchi hiyo ili lengo la kuanzisha Chuo hicho liweze kutimia.

Amesema kwa kuwa Chuo cha Teknolojia cha India kimepiga hatua ya juu zaidi katika masuala ya Teknolojia hivyo ujio wa ujumbe huo ni hatua ya kuona mazingira ya nchini kwetu katika kutimiza adhma yao ya kuanzisha chuo hapa nchini.

“Wenzetu hawa wanataka kuanzisha Chuo hapa nchini tuliwaalika waje na tayari wamefanya mazungumzo na Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar na kuahidiwa ardhi kwa ajili ya kuazisha huko, lakini kwa kuwa suala la elimu ya juu ni la muungano tunaangalia taratibu za urekebu kuona nini kinaweza kufanyika ili kazi hii iweze kuanza,”amesema

“Wanataka kuanza kuchukua wanafunzi mwezi Oktoba mwaka huu ni muda mfupi sana kutokea sasa ila tutafanya kazi usiku na mchana kuona ni nini kinaweza kufanyika tukasonga mbele,”amesema

Waziri Mkenda Amesema pia timu hiyo kutoka India imekwenda kutembelea Chuo Kikuu cha Afrika cha Nelson Mandela kilichoko jijini Arusha pamoja na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) ili kuona vifaa vya kujifunzia na kufundishia vilivyopo na namna ambavyo wanaweza kufanya kazi kwa pamoja.

“Timu hii tutakutana nayo tena Februari 17 mwaka huu ili kwa pamoja tuangalie rasimu ya makuballiano (MOU) ili tuone tunakwendaje,” alisema Waziri Mkenda

Kwa upande wake Balozi wa India nchini Tanzania Binaya Pradhan Serikali ya India imejizatiti (committed) kufanya kazi na Serikali ya Tanzania ili kuhakikisha pamoja na mabo mengine lengo la kuanzia Chuo nchini Tanzania linafanikiwa.

Post a Comment

0 Comments