Watanzania wametakiwa kuendelea kuwaenzi Mashujaa wa Vita vya Majimaji kwa kuhifadhi mila na tamaduni zao kwa kufanya kazi kwa bidii, kulinda rasilimali za Taifa, kupambana na kuzuia rushwa, madawa ya kulevya pamoja na ujangili wa wanyamapori
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) ameyasema hayo leo katika Kilele cha Tamasha la Kumbukizi la Vita vya Majimaji na Utalii wa Utamaduni lililofanyika Mjini Songea.
Ameeleza kuwa haitakuwa na maana yoyote ya kujipambanua kuwa tunaenzi Mashujaa wetu wa vita vya Maji Maji ilhali maadili na rasilimali tulizorithi kutoka kwao zikiendelea kuporomoka na kupotea.
Akizungumza kuhusu umuhimu wa tamasha hilo, Mhe. Masanja amesema Kumbukizi ya Vita ya Majimaji ni tunu ya Taifa kwa vile inakiwezesha kizazi cha sasa na cha baadae kuendelea kuona na kujifunza namna ambavyo baadhi ya Watanzania wamekuwa wakijitolea maisha yao katika kupigania uhuru,kulinda na kuhakikisha rasilimali za Taifa zinatumika kwa maslahi ya umma.
Aidha, Ametoa wito kwa watanzania kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kutumia kumbukumbu hizo kama vyanzo vya ajira ili ziendelee kuchangia katika vita dhidi ya adui umaskini kama ambavyo zilitumika kupigana vita dhidi ya uvamizi wa wakoloni.
Akizungumzia kuhusu ombi la kurejeshwa kwa fuvu la Songea Mbano aliyekuwa mmojawapo wa Mashujaa wa Vita vya Majimaji lililochukuliwa na Wajerumani, Mhe.Mary Masanja amefafanua kuwa tayari Kamati ya kitaalam ya kuratibu zoezi hilo imeanza kubainisha malikale zote za Tanzania zilizopo nje ya nchi kwa ajili ya kuzirejesha hapa nchini
Tamasha hilo lililohudhuriwa viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali, viongozi wa dini, machifu na wananchi kutoka maeneo mbalimbali lilikuwa na Kauli mbiu ya “MAKUMBUSHO YA MAJIMAJI NI URITHI WETU, TUYAHIFADHI KWA MAENDELEO YA UTALII NA UCHUMI”
0 Comments