Na Mwandishi Wetu
TAASISI ya FEET imetoa mafunzo ya ujasiriamali kwa wasichana wanaosoma Shule ya Sekondari Ahmes iliyopo Bagamoyo mkoani Pwani, lengo likiwa kuwajengea uwezo wa namna ya kuanza kufahamu mbinu , mikakati na mipango inayowezesha wasichana kujikita katika ujasiriamali.
Akizungumza na waandishi wa habari Mmoja wa waratibu wa programu ya Wasichana na ujasiriamali kutoka FEET Safia Hashim amesema katika Shule hiyo wanafunzi wa kike 86 wamenufaika na mafunzo hayo kupitia kempu ya mafunzo hayo na lengo ni kuwafikia wanafunzi wengi zaidi wa kike.
"Lengo la kuwa na program ya ujasiriamali kwa wasichana shuleni ni kuendelea kuhamasisha wanafunzi wa kike kupenda ujasiriamali na sio tu kufikiria masuala ya taaluma nyingine peke yake.Tumeanza na Shule hii lakini tutakwenda na shule nyingine.
“Matarajio ya FEET ni kuhakikisha wanafunzi wa kike baada ya kumaliza elimu yao wasiwe na fikra za kusubiri kuajiriwa bali wanaweza kujiajiri kwa kufanya shughuli za ujasiriamali,”amesema.
Alipoulizwa sababu za kuwa na programu hiyo,amesema ni baada ya kugundua wasichana wengi hawajui namna ya kuanzisha biashara lakini baada ya kupata uelewa wanaweza kuwa na biashara zao na kujua nini wafanye ili wafanikiwe.
Kwa upande wake Humphrey Ottaru ambaye ni moja ya waratibu wa program hiyo na mtoa mada kutoka FEET amesema wameona Kuna kila sababu ya kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa wanafunzi wa kike walioko shuleni kama njia mojawapo ya kuwandaa na kuwafanya wajiamini
Wakati huo huo akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake , mwanafunzi Deborah Munuo mwanafunzi wa kidato cha tano mwenye ndoto za kuwa daktari wa moyo amesema amefurahishwa na mafunzo ya ujasiriamili,kwani wamefundishwa kujitegemea , kupambania ndoto na kuweka mikakati kuhusu biashara wanazotaka kuanzisha.
“Pia tumejifunza tabia ya kuweka fedha na kutunza ili kutimiza malengo kwenye maisha yangu, pamoja na hayo nimejifunza ya kwamba ukiachana na ndoto yangu ya kuwa daktari ninaweza kujihusisha na ujasiriamali na unaweza kupata kipato kikubwa katika maisha yangu, hivyo ningependa kuishauri taasisi ya FEET kuendelea na huu mchakato wa semina ya ujasiriamali kwa vile ni ukombozi kwa binti wa kitanzania.
Naye mwanafunzi mungine wa kidato cha tano shule hapo Kunty Shaban amesema mafunzo ya ujasiriamali kwa wasichana imekuwa ya kipekee kwao kwani imekuwa na ukombozi kwa wasichana wanaosoma shuleni hapo.
“Semina ambayo nimeipata imenigusa moja kwa moja kwani nasoma uchumi na natamani mafunzo haya yaendelee kwenye shule nyingine ili wasichana wangi waelimishwe.”
Ameongeza kupitia semina ya ujasiriamali kwa wasichana imemfanya aongeze kujiamini, kujisimamia na kujitambua lakini kufahamu mambo muhimu yanayomzunguka mwanamke.
“Semina ya ujasiriamali kwa wasichana iliyotolewa na FEET imenidhihirishia jinsi gani wasichana tunatambulika , tunathaminiwa kwenye jamii na kwamba tunaweza kufanya mambo makubwa, mfano mzuri ni mama yetu Rais Dk.Samia Suluhu Hassan.
“Rais wetu ametuonesha mfano mkubwa kwa mambo makubwa ambayo ameyafanya mpaka sasa katika maeneo mengi na hii inatupa nguvu zaidi watoto wa kike wote Tanzania na hata wanawake wengine Afrika kuona jinsi gani tulivyo na nguvu,”amesema.
Hivyo ametoa ombi kwa FEET waendelee kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa wanafunzi wengi zaidi wa kike maana ni ukombozi kwa wasichana wote Tanzania ,Afrika na hata ulimwenguni.
Kuhusu miaka miwili ya Rais Dk. Samia, amesema wanampa pongezi kwa kuwa mwanamke wa kwanza kushika cheo cha urais, wanampongeza kwa vitu vyote alivyovifanya.
“Najua Rais amefanya vitu vingi, siwezi kutaja vyote lakini huduma kwa watoto wa kike shuleni, huduma za kiafya hospitalini , anavyotembelea na kujali anawaongoza inatia moyo na utendaji wake unafanya na wengine kutimiza wajibu wao inavyopasa.
"Kwa namna ya kipee tunapenda kumshukuru na kumpa pongezi na tunatumaini kwa muda alionao na hata atakapoongezewa tunategemea mambo makubwa.Kwa hiyo pongezi kwako Rais Samia Suluhu Hassan.”
0 Comments