Ticker

6/recent/ticker-posts

NAMIBIA YAVUTIWA NA TANZANIA INAVYOKABILIANA NA TATIZO LA AJIRA


Na Mwandishi Wetu, DODOMA

UJUMBE wa Bunge la Namibia umeimwagia sifa Serikali ya Tanzania namna ilivyojipanga kukabiliana na tatizo la ajira kwa vijana kupitia programu zinazotekelezwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.

Kiongozi wa ujumbe huo na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge hilo ya Rasilimali watu na Maendeleo ya Jamii ambaye pia ni Mbunge, Mhe. Nono Katjingisua, ametoa pongezi hizo leo Machi 30, 2023 baada ya kukutana na Mofisa wa Ofisi hiyo wakiongozwa na Kaimu Katibu Mkuu ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Hifadhi ya Jamii, Festo Fute.

Mhe.Katjingisua amesema Serikali ya Namibia mwaka 2022 ilikumbwa na tatizo la ajira kwa vijana hivyo hali hiyo imewasukuma kuja Tanzania kujifunza namna inavyokabiliana na tatizo hilo.

“Tumepata maelezo ambayo na sisi tutakaporejea bungeni tutazingatia kama vile kuwa na program ya taifa ya kukuzaji ujuzi ili kuwajengea uwezo vijana kupata ujuzi utakaowasaidia kujiajiri au kuajiriwa kulingana na mahitaji ya soko la ajira,tumeona wenzetu wana mfuko wa maendeleo ya vijana ambao unatoa mitaji kwa vijana, tumejifunza mengi,”amesema.

Naye, Mjumbe wa Kamati hiyo ya Bunge, Tjiveze, Herlinde, amevutiwa na Tanzania inavyofanya jitihada mbalimbali za kuwakwamua vijana ikiwamo kutunga sheria ya manunuzi ya umma inayoelekeza asilimia fulani ya zabuni iwe ya vijana na namna inavyowajumuisha vijana wenye ulemavu kwenye fursa zilizopo za ajira.

Awali, akiwaongoza Maofisa wa Ofisi ya Waziri Mkuu kueleza namna inavyotekeleza program za vijana na uratibu wa ajira, Mkurugenzi wa Idara ya Hifadhi ya Jamii, Festo Fute, amesema ofisi hiyo ni mratibu mkuu wa masuala ya vijana na kuna sera ya vijana ambayo kwasasa inafanyiwa mapitio ili iendane na wakati.

Post a Comment

0 Comments