Ticker

6/recent/ticker-posts

TANZANIA NA MAREKANI ZAKUBALIANA UWEKEZAJI MKUBWA KWENYE UTALII NCHINI.


Na John Mapepele

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa leo Machi 23, 2023 amekutana na ujumbe wa Serikali ya Marekani ulioongozwa na Balozi wa Marekani hapa nchini, Mhe. Michael Battle na kukubaliana kusaini mikataba ya kufanya uwekezaji mkubwa kwenye Sekta ya Utalii hapa nchini.

Mazungumzo hayo yamefanyika katika ofisi za Wizara hiyo zilizopo jijini Dodoma ambapo pande zote mbili zimekubaliana kuisaini mikataba hiyo baada ya kuweka sawa maeneo machache ya mikataba hiyo ambayo pande hizo zilikuwa zikivutana.

Aidha, katika kikao hicho ambacho kilihudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi pande zote zimekubaliana kuyapitia maeneo hayo kwa haraka ili iweze kusainiwa katika muda mfupi ujao.

"Nina furaha kuona kuwa kimsingi tumekubaliana mambo ya uwekezaji mkubwa, kuna mambo machache tu tumevutana kidogo kwa manufaa ya nchi yetu ambayo pia tumekubaliana kila pande iende kuweka vizuri ili tukamilishe zoezi hili kwa wakati." Amesisitiza Mhe. Mchengerwa

Akifafanua, Mhe. Mchengerwa amesema katika kikao hicho pia wamejadiliana kuhusu namna gani wawekezaji kutoka Marekani watawekeza nchini katika maeneo yaliyohifadhiwa yanayosimamiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii.

Ameongeza kuwa tayari Wizara imeipatia Serikali ya Marekeni vipaumbele vya Taifa ili iweze kujipanga vizuri katika eneo la kuwekeza katika Sekta ya Utalii hapa nchini.

Amesema imani waliyonayo kama Serikali endapo wakifanikiwa tukiondoa kero chache zilizopo katika mkataba, Serikali itaweza kuingiza fedha nyingi kupitia Sekta ya Utalii kuliko kipindi chochote.

Akifafanua zaidi amesema " kwa sasa ni takribani dola milioni 1.5 zinazoingizwa kutokana na utalii kwa lakini baada ya kuridhiana na kuingiza kwenye mikataba hiyo Serikali itaweza kuingiza hadi dola milioni 11 katika kipindi cha mwaka mmoja".

Aidha, amepongeza kazi kubwa iliyofanywa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kuitangaza Tanzania kupitia Filamu ya Royal Tour ambapo amesisitiza kuwa kutokana na kazi kubwa aliyoifanya na Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan idadi ya watalii imeongezeka ambapo hadi kufikia mwezi Februari mwaka huu Tanzania imepokea watalii milioni 1.8 kutoka nje ya nchi, rekodi ambayo haijawahi kufikiwa toka uhuru wa Tanzania na wakiongezwa idadi ya watalii wa ndani Tanzania imepata jumla ya watalii milioni 5 katika kipindi hiki.

Pia, Mhe. Mchengerwa amesema mbali na mijadala waliyoifanya leo tayari Serikali ya Tanzania imekuwa na uhusiano wa muda mrefu na Serikali ya Marekani katika maeneo mbalimbali ikiwa la kupambana na uhalifu na majangili wa uwindaji haramu katika maeneo yaliyohifadhiwa.

Aidha, amesema anaamini kazi kubwa imefanywa na Serikali ya kuitangaza Tanzania ikiongozwa na Mhe Rais Samia Suluhu Hassan ambapo amesema kazi inayotakiwa kufanyika kwa sasa ni kuongeza miundombinu ya maeneo ya kufikia watalii yenye viwango vya kimataifa kama mahoteli.

Naye Balozi Michael Battle amempongeza Rais Samia kwa kutoka na kufanya filamu ya Tanzania The Royal Tour ambapo amesema imeleta faida kubwa ya kuongeza idadi ya watalii nchini.

Aidha amesema nchi yake itaendelea mashirikiano na Tanzania katika kuhifadhi raslimali na kuwekeza kwenye Utalii.

Post a Comment

0 Comments