Mhadhiri Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Dkt. Neema Mduma
Mhadhiri kutoka Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Dkt. Neema Mduma ametoa wito kwa wanawake walio katika sekta ya TEHAMA kutumia ujuzi wao kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii.
Dkt. Neema ameyasema hayo Machi 29, 2023 katika mahojiano maalum na televisheni Mtandao ya TCRA yaliyoongozwa na Mtangazaji Barbara Hassan kupitia mada ya Ujasiriamali kupitia Tehama.
" Natoa wito kwa wanawake wenzangu waliopo katika sekta ya TEHAMA kutumia teknolojia ili kuleta maendeleo na kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii" amesema Dkt. Neema
Aidha ameeleza kuwa, Taasisi ya Nelson Mandela ipo mstari wa mbele katika kuwainua sekta ya TEHAMA kupitia CENIT@EA imeweza kufadhili wanafunzi kutoka nchi za Afrika Mashariki kupata elimu na ujuzi katika sekta hiyo.
" Katika kuonesha kuwa wanawake wamedhamiria kuleta ufumbuzi kwa jamii kupitia TEHAMA wanafunzi watatu wa kike kutoka katika Taasisi yetu wamefanikiwa kuja na bunifu ya Smart Ugali Cooker inayorahisisha upikaji wa chakula hicho" amesema Dkt. Neema.
Dkt. Neema ametoa mfano wa wanawake watatu ambao wamechangia katika ujasiriamali kupitia TEHAMA ambao ni pamoja na Dr Dina Machuve - mmoja wa waanzilishi wa Asasi isiyo ya kiserikali ambayo imelenga kutumia teknolojia ya mashine ya kujifunzia ( Machine Learning) katika kutatua matatizo mbalimbali ya jamii ikiwemo kutengeneza mifumo ya kugundua magonjwa yanayoshambulia kuku na kutafuta suluhisho na Bi. Rose Funja Mkurugenzi na Muanzilishi wa Agriinfo ambayo imelenga kutumia teknolojia ya drones au ndege zisizo na rubani katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakumba wakulima .
Vilevile, Bi.Carol Ndosi Mwanzilishi wa the Launchpad Tanzania ambae amejikita katika kusuka agenda ya mitandao salama na wanawake katika teknolojia.
0 Comments