TIMU ya Benki ya Dunia imeanza ziara maalum ya kufuatilia utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) na kufanya majadiliano ili kuhakikisha mradi unafikia malengo yake.
Akizungumza katika kikao cha pamoja na Timu hiyo ya Benki ya Dunia Jijini Dar es Salaam kwa njia ya mtandao kutokea Dodoma, Naibu Katibu Mkuu Prof. James Mdoe ameihakikishia Benki ya Dunia kuwa Wizara inaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ambao unalenga pamoja mambo mengine kuleta mageuzi makubwa na kuongeza fursa katika elimu ya juu.
Prof. Mdoe ameeleza kuwa Mradi huo wa HEET unatekelezwa katika Taasisi 22 pamoja na Wizara, na kwamba katika kikao kinachofanyika wizara imewasilisha taarifa ya jumla ya utekelezaji pamoja na kujadili changamoto zilizojitokeza katika kipindi cha awali cha utekelezaji.
Aidha, ameongeza kuwa taasisi zote zinazotekeleza mradi huo zitapa nafasi ya kutoa taarifa za utekelezaji kwa kina na kufanya majadiliano nao na kwamba timu hiyo kutoka Benki ya Dunia itapata fursa ya kutembelea baadhi ya maeneo ya utekelezaji wa mradi.
Naye Kiongozi wa Timu ya Benki ya Dunia Roberta Bassett amesema lengo la kufanya ziara hiyo ni kuangalia utekelezaji wake na kuona kama kuna changamoto zozote ili waweze kutoa ushauri na kuona ni namna gani wanaweza kusaidia kufanikisha mradi kutekelezwa kwa wakati na ufanisi.
Timu hiyo itakuwa na ziara katika baadhi ya maeneo ambapo mradi huo unatekelezwa ambayo ni Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius Nyerere cha Kilimo na Teknolojia na Kampasi ya Chuo Kikuu cha Ardhi iliyopo Sengerema baada ya kupokea taarifa za utekelezaji kutoka kwa taasisi zote zinazotekeleza mradi huo.
Mradi wa HEET unafadhiliwa na Benki ya Dunia na una thamani ya Dola za kimarekani Milioni 425 sawa na Shilingi Bilioni 972 za Tanzania, pamoja na mambo mengine unawezesha kujenga kampasi 14 mpya za Vyuo vikuu katika Mikoa 14 ikiwemo Tanga, Lindi Kigoma, Tabora, Ruvuma, Manyara, Simiyu, Kagera, na Zanzibar
0 Comments