Ticker

6/recent/ticker-posts

KAMATI YA BUNGE YAIPONGEZA REA NA KUHAMASISHA WANANCHI KUCHANGAMKIA FURSA ZA UMEME VIJIJINI


Veronica Simba na Issa Sabuni - REA

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imesema imeridhishwa na utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini mkoani Singida na imewashauri wananchi wanaoishi vijijini waliofikiwa na huduma ya umeme, kuitumia nishati hiyo kwa matumizi yenye tija hususani katika shughuli za kujiongezea kipato na kukuza uchumi.

Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Irisya wilayani Ikungi, Mkoa wa Singida, wakati wa ziara ya Kamati hiyo kukagua maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili (R3R2), Aprili Mosi 2023, Makamu Mwenyekiti wa PIC, Augustino Vuma amesema lengo la Serikali kupeleka umeme vijijini ni kuwarahisishia wananchi kutekeleza kwa ufanisi shughuli mbalimbali za kiuchumi ili wajiletee maendeleo hivyo kutoitumia nishati hiyo ni kurudisha nyuma juhudi hizo za Serikali.

“Nitoe rai kwa wananchi kuitumia vizuri fursa hii ya uwepo wa umeme kwa kubuni shughuli mbalimbali za kiuchumi ili sasa ile dhana ya Serikali kuleta umeme hapa iweze kuonekana kwa maana ya kuchochea ukuaji wa uchumi na faida nyinginezo,” amesisitiza.

Aidha, Makamu Mwenyekiti amewaagiza Watendaji wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuendelea kuwasimamia kwa ukaribu wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini ili kuhakikisha wanafanya kazi kwa kuheshimu mikataba yao na kufanikisha azma ya Serikali kuwafikishia umeme wananchi wote waishio vijijini waweze kujikwamua kiuchumi.

Katika hatua nyingine, Makamu Mwenyekiti wa PIC ameeleza kuwa Kamati imeridhishwa na utekelezaji wa Mradi wa R3R2 huku akibainisha kuwa tayari manufaa yake yamekwishaanza kuonekana.




“Leo tumekuwa hapa katika Shule ya Sekodari Irisya na tumeshuhudia kwa macho yetu kwamba wanafunzi wameshaanza kunufaika kwani umeme umeingia kwenye Maabara na kufika katika madarasa hivyo kuwawezesha kujisomea hata nyakati za usiku.”

Akifafanua zaidi, amesema Kamati imeshuhudia uwepo wa umeme katika Maabara ya Fizikia na nyinginezo na kuwawezesha wanafunzi kusoma kwa vitendo. Amesema kuwa, kupitia uwepo wa umeme, matarajio ni kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wa masomo ya sayansi na kwamba ufaulu katika masomo yote pia utaongezeka kwani mazingira yameboreshwa.

Vilevile, ameongeza kwamba kuhusu manufaa kwa wananchi, umeme umeanza kuwafikia hivyo wataweza kufanya shughuli za kiuchumi ikiwemo kuanzisha viwanda vidogo vidogo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Janet Mbene pamoja na kuunga mkono uhamasishaji wananchi kuunganisha umeme katika makazi na shughuli za kiuchumi, amesema ni faraja kwa REA kuona umeme unaendelea kuwafikia wananchi katika maeneo mbalimbali vijijini.

“Lengo letu ni lilelile, kuhakikisha kwamba kila kijiji kinapata umeme na hatimaye uwasaidie wananchi kiuchumi, kijamii na hata kimaendeleo kwa maana ya elimu na vitu vingine,” amesisitiza.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mbele ya Kamati ya PIC, Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba na Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Irisya, Ernest Edward wametoa shukrani kwa Serikali kupitia REA kwa kufikisha umeme katika kijiji hicho.

Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini mkoani Singida kwa Kamati, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy ameeleza kuwa Serikali kupitia Wakala hiyo imetoa jumla ya shilingi bilioni 73.1 na Dola za Marekani 988,707.60 ili kuhakikisha miradi minne inayotekelezwa mkoani humo inakamilika na wananchi wanapatiwa huduma ya nishati hiyo ili kujipatia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Aidha, ameeleza zaidi kuwa Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili katika Wilaya za Ikungi na Singida unatekelezwa na Mkandarasi M/s Central Electricals International Ltd kwa gharama ya shilingi bilioni 26.3 na katika Wilaya za Iramba, Manyoni na Mkalama, unatekelezwa na M/s CRJE – CTCE Consortium kwa gharama ya shilingi bilioni 31.6




Amesema kuwa, maendeleo ya Mradi kwa wastani yamefikia asilimia 70.21 ambapo kwa Wilaya za Ikungi na Singida, Mkandarasi amefikia asilimia 77.54 na Wilaya za Iramba, Manyoni na Mkalama, Mkandarasi amefikia asilimia 62.87

Mkoa wa Singida una jumla ya vijiji 441 ambapo vijiji 287 vimekwishapatiwa umeme kupitia miradi ya umeme vijijini iliyotekelezwa awali. Vijiji 169 vilivyobaki vinaendelea kuunganishiwa umeme kupitia Wakandarasi waliotajwa.

Post a Comment

0 Comments