Na John Mapepele
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka watekelezaji wote wa Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii kusini (REGROW) kuondoa ukiritimba wakati wa kutekeleza mradi huu ili kukuza na kutangaza mazao mapya ya utalii katika mikoa ya kusini mwa Tanzania vinginevyo hatua kali zitachukuliwa kwa watakaobainika kufanya uzembe au kuuhujumu mradi huo.
Mhe. Mchengerwa ametoa kauli hiyo leo Aprili 16, 2023 jijini Arusha wakati akitoa hotuba yake kwenye hafla ya utiaji saini mikataba nane ya ujenzi wa miundombinu yenye thamani ya shilingi bilioni 157.29 chini ya mradi wa kuboresha usimamizi wa Maliasili na kukuza utalii kusini mwa Tanzania.
“Wanaopaswa kwenda kusimamia lazima waende wakasimamie na watendaji ambao watabainika kutofanya vizuri watachukuliwa hatua, dhamira ya serikali ni kuhakikisha kuwa tunafanya vizuri ili twende tukapate fedha zaidi katika awamu ya pili.” Amesisitiza Mhe. Mchengerwa
Waziri Mchengerwa amewataka wakandarasi wote waliosaini mikataba hiyo kutumia vizuri muda waliopewa kwa kufanya kazi nzuri katika muda mfupi na kwamba wasitarajie kuongezewa muda.
Mikataba iliyosainiwa imegawanyika katika makundi mawili; mikataba minne ya ujenzi wa majengo pamoja na mikataba minne ya ujenzi wa viwanja vya ndege ambayo itatekelezwa katika hifadhi nne za Ruaha, Mikumi Udzungwa na Nyerere na Msitu wa Asili wa Kilombero chini ya TFS .
Akifafanua zaidi amesema kwenye mikataba ya ujenzi wa viwanja inatarajiwa viwanja sita vya ndege kujengwa ambapo viwanja vitatu vya ndege vitajengwa hifadhi ya Ruaha , viwanja viwili hifadhi ya Mikumi na hifadhi ya Nyerere kitajengwa kiwanja kimoja cha ndege.Aidha amesema katika hifadhi ya Udzungwa kutajengwa njia ya juu ya watalii ambayo inakadiriwa kuwa na kilomita moja ambayo inatarajiwa kuwa miongoni mwa njia ndefu zaidi Afrika Mashariki na hata kusini mwa Afrika itakapokamilika.
Mhe. Mchengerwa amefafanua kuwa miundombinu mbalimbali kama vile majengo ya utalii, mageti, vituo vya habari, nyumba za watalii, hosteli vituo vya askari pamoja na maeneo ya kupumzikia yatajengwa ili kuhakikisha watalii wanafurahia wanapotembelea katika maeneo hayo.
Amesema ujenzi wa miradi hii itasaidia kufungua fursa na kukua kwa uchumi wa mikoa ya kusini na amewaomba wakazi wa mikoa ya kusini kuchangamkia fursa wakati wa utekelezaji wa miradi.
Aidha, Mhe.Mchengerwa ametoa wito kwa wananchi wa Mikoa ya Kusini kuchangamkia fursa za ajira zitakazotokana na utekelezaji wa mikataba hiyo ambapo amewasisitiza watakaopata kazi hizo wakawe wazalendo na wafanye kazi kwa bidii ili kwa pamoja mradi huo uweze kuchagiza maendeleo ya ukuaji wa Sekta ya Utalii pamoja na kukuza kipato cha mwananchi mmoja mmoja.
Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi ameelezea kusikitishwa kwake kwa jinsi ambavyo mradi umekuwa ukishindwa kutekelezwa bila sababu zozote za msingi ambapo hadi Machi mwaka huu mradi huo umetekelezwa kwa asilimia 43 tu na kuonya kuwa hatamfumbia macho mtekelezaji yoyote wa mradi huo.
Mradi REGROW ulianzishwa mwaka 2017 kwa lengo la kupanua wigo wa mazao ya utalii kijiografia kwa kuendeleza Sekta ya Utalii katika Mikoa ya Kusini.
Mradi huo unatekelezwa kupitia fedha za mkopo wa masharti nafuu wa Dola za Marekani Milioni 150 kutoka Benki ya Dunia.
0 Comments