Meneja wa OSHA Kanda ya Kusini Bw. Wilbert Ngowi akitoa elimu ya masuala ya usalama na afya katika uchimbaji na uchukuzi wa makaa ya mawe kwa wafanyakazi na viongozi wa kampuni za BECCO na ARIA Commodities Mkoani Ruvuma.
Viongozi na Wafanyakazi wa Kampuni za ARIA Commodities na BECCO Limited wakifuatilia mada ya masuala ya usalama na afya mahali pa kazi kutoka kwa Meneja wa OSHA Kanda ya Kusini Bw. Wilbert Ngowi (hayupo pichani)
Meneja wa OSHA Kanda ya Kusini Bw. Wilbert Ngowi akijibu swali kutoka kwa mfanyakazi wa BECCO Limited aliyeuliza kuhusu namna sahihi ya kujikinga dhidi ya vumbi la makaa ya mawe katika maeneo ya ofisi na mgodi.
Mfanyakazi wa Kampuni ya uchimbaji wa Makaa ya mawe ya JITEGEMEE Limited akiuliza swali kwa Meneja wa OSHA Kanda ya Kusini Bw. Wilbert Ngowi (hayupo pichani) kuhusu njia sahihi za kuzuia na kudhibiti vihatarishi katika maeneo yao ya migodi.
************************
Na Mwandishi wetu
Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) umetoa wito kwa wawekezaji na waajari wa sekta ya makaa ya mawe kuhakikisha wanazingatia ipasavyo sheria na miongozo ya usalama na afya ili kuwalinda wafanyakazi wao dhidi ya ajali na magonjwa yanayoweza kuwapata katika maeneo yao ya kazi.
Wito huo umetolewa kupitia kwa Meneja wa OSHA Kanda ya Kusini, Bw.Wilbert Ngowi alipokuwa akihitimisha programu maalumu ya siku nne ya mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi kwa Viongozi na Wafanyakazi wa sekta ya makaa ya mawe Wilayani Mbinga Mkoani Ruvuma.
“Sekta ya makaa ya mawe inakabiliwa na vihatarishi mbalimbali kama ilivyo kwa sekta zingine za madini mfano mfanyakazi anapovuta vumbi la makaa kwa muda mrefu anaweza kupata ugonjwa wa nimonia ya mapafu meusi (coal worker’s pneumoconiosis), ugonjwa huu hauna dalili za haraka wala tiba hivyo mfanyakazi akiathirika na huu ugonjwa utakuwa ndio ulemavu wake wa maisha na pengine unaweza kumsababishia kifo,”
“Hivyo basi kutokana na sekta hii kukabiliwa na vihatarishi vingi na vinavyoweza kuhatarisha Maisha ya wafanyakazi tumeona tuanze kuchukua tahadhari mapema kwa kuendesha programu maalumu ya mafunzo kwa lengo la kuwapa elimu wafanyakazi hawa ili waweze kuepukana na vihatarishi hivi vya ajali na magonjwa vinavyoweza kuwapata katika maeneo yao ya kazi ikiwa ni pamoja na kuepukana na vumbi la makaa ya makaa ya mawe”. Alisema Bw. Ngowi akiongeza kwa kutoa wito kwa wawekezaji.
“Nitoe wito kwa Waajiri na Wawekezaji wa Sekta ya Makaa ya Mawe wahakikishe kwamba wanazingatia taratibu zote za usalama na afya katika maeneo yao yote ya kazi kwa kuchukua tahadhari zote stahiki ikiwa ni pamoja na kuhakikisha vumbi linapungua katika maeneo yao pia wahakikishe vifaa vyote vinavyotumika katika shughuli mbalimbali vinamkinga mfanyakazi dhidi ya vihatarishi vya ajali na magonjwa.” aliongeza Bw. Ngowi.
Aidha kupitia progamu hiyo ya mafunzo, Mkurugenzi wa Oparesheni wa Kampuni ya uchimbaji wa Makaa ya mawe ya Jitegemee Holdings, Bw.Boscow Mabena ameeleza namna ambavyo kampuni hiyo imehamasika katika kuimarisha mifumo ya usalama na afya katika Kampuni yake.
“Tunawashukuru sana OSHA kwa kutupatia elimu hii ya usalama na afya katika sekta yetu ya makaa ya mawe, wamekuwa wakitutembelea na kutupa miongozo mbalimbali ya namna sahihi ya kuboresha mazingira ya kazi hivyo tumehamasika kwa kiasi kikubwa sana na tayari tumetenga bajeti ya mafunzo ya usalama na afya, tutapeleka wafanyakazi wakahudhurie mafunzo hayo yanayotolewa na OSHA” alisema Bw. Mabena.
Kwa upande wao washiriki wa mafunzo hayo kutoka kampuni mbalimbali wanaeleza namna ambavyo elimu hiyo itawaongezea tija katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
“Nime elimika kwa kiasi kikubwa sana na kama kiongozi itanisaidia kuwasimamia vyema wafanyakazi wenzangu katika eneo letu la kazi ikiwemo kuwalinda dhidi ya vumbi la makaa ya mawe linaloweza kusababisha ugonjwa wa nimonia ya mapafu meusi vivilevile tunaahidi kutekeleza mambo yote yaliyoagizwa na sheria ya usalama na afya ikiwemo kuhakikisha wafanyakazi wote wana tekeleza majukumu yao wakiwa wamevaa vifaa kinga.” Alisema Rajabu Miraji
Kwa upande wake Bi. Merce Gerald ambaye ni Mhandisi kutoka Kampuni ya Jitegemee ameeleza kuwa mafunzo haya yataleta mabadiliko ya kiusalama kwa kiasi kikubwa sana katika maeneo yao ya kazi.
“Elimu hii itatusaidia sana kujikinga na vihatarishi mbalimbali tunavyokabiliana navyo katika maeneo yetu ya kazi hivyo niombe OSHA waendelee kutoa mafunzo haya kwa migodi mingine ili waweze kuokoa Maisha ya wafanyakazi wengine wa sekta hii.”alisema Bi. Merce Gerald.
Programu hii maalumu ya mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi katika sekta ya uzalishaji wa makaa ya mawe imefanyika kuanzia tarehe 11 – 14/04/2023 na jumla ya wafanyakazi 400 kutoka kampuni za TANCOAL, RUVUMA COAL, JITEGEMEE HOLDINGS, ARIA COMMODITIES na BECCO LTD wamefikiwa na elimu hiyo.
0 Comments