Mkaguzi wa usalama wa mifumo ya umeme wa OSHA, Mhandisi Maria Ndaskoy akifanya ukaguzi wa mifumo ya umeme katika jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Morogoro.
Meneja wa OSHA Ofisi ya Kanda ya Pwani, Mhandisi, George Chali (kushoto) akizungumza na watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Morogoro, wakati wa kikao cha kutoa mrejesho wa ukaguzi uliofanywa na OSHA katika ofisi na maeneo mbalimbali ya jengo hilo.
Mkaguzi wa afya na mazingira ya kazi wa OSHA, Bw. Renatus Qalqal akifafanua namna sahihi ya matumizi ya kiti cha egonomia katika ofisi wakati akitoa mrejesho wa ukaguzi uliofanywa na OSHA katika jengo hilo la Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro.
Mkaguzi wa usalama wa umeme wa OSHA, Mhandisi Maria Ndaskoy akifafanua jambo kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro, Mhe.Jaji. Paul Ngwembe wakati akitoa mrejesho wa ukaguzi wa mifumo ya umeme uliofanywa na OSHA katika jengo la Ofisi hizo.
****************
Na Mwandishi Wetu
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe, ametoa wito kwa viongozi wa Taasisi mbali mbali za umma kushirikiana na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) katika kuhakikisha kwamba miundombinu iliyowekezwa na serikali katika Taasisi zao pamoja na usalama wa wafanyakazi vinalindwa.
Ametoa kauli hiyo mara baada ya kuhitimishwa kwa zoezi la ukaguzi wa mifumo ya usalama na afya katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Mkoani Morogoro ambao umefanyika sambamba na mafunzo ya kuwajengea uelewa wa masuala ya usalama na afya watumishi wa Mahakama hiyo.
“Kwa kipindi cha hivi karibuni serikali imewekeza fedha nyingi sana katika ujenzi wa Ofisi bora za Mahakama hapa nchini na zaidi ya hapo serikali imejenga Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki (Integrated Justice Centres) zenye mahakama za ngazi zote kuanzia Mahakama ya Mwanzo pamoja na ofisi mbali mbali za wadau wote wa Mahakama wakiwemo Mawakili wa Kujitegemea zipatazo sita (6) nchi nzima. Hivyo, sisi kama viongozi tunatambua umuhimu wa kuhakikisha kwamba uwekezaji huu wa serikali unatunzwa ipasavyo ili miundombinu hiyo iweze kutumika kwa kipindi kirefu zaidi,” ameeleza Mheshimiwa Ngwembe na kuongeza kuwa:
“Jambo hili ndilo limetufanya sisi kuona kuna haja ya kushirikiana na wenzetu wa OSHA ambao ndio wataalam wa masuala ya usalama na afya mahali pa kazi ili kuweza kupata ushauri endelevu katika kulinda afya za wafanyakazi pamoja na miundombinu yote muhimu katika Ofisi zetu za Mahakama.”
Aidha, Kiongozi huyo Mkuu wa Mahakama Kanda ya Morogoro amebainisha kwamba Ofisi yake itaendelea kushirikiana na OSHA katika kuhakikisha kwamba ukaguzi wa mifumo ya usalama na afya pamoja na mafunzo kwa watumishi wa Mahakama unakuwa endelevu na unafanyika katika Ofisi zote za Mahakama katika kanda husika.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amewapongeza Viongozi wa Mhimili wa Mahakama kwa kutambua umuhimu wa kulinda miundombinu bora ya Ofisi za Mahakama kupitia utekelezaji wa taratibu zote muhimu za utunzaji wa majengo ikiwemo kuhakikisha majengo hayo yanakuwa na mifumo madhubuti ya usalama na afya.
“Ninaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufanya uwekezaji mkubwa katika miundombinu bora ya Ofisi za Mahakama nchini jambo ambalo litafanikisha azma yake ya kuharakisha utoaji wa haki kwa wananchi kupitia chombo hiki muhimu cha Mahakama. Aidha, pongezi hizi ziwaendee viongozi wa Mhimili wa Mahakama kwa kutambua thamani ya uwekezaji huo na kushirikiana nasi ili kuhakikisha kwamba uwekezaji huo unabaki salama wakati wote. Lengo la kaguzi za OSHA sio tu kumlinda mfanyakazi lakini vile vile ni kulinda uwekezaji ili kuwa na uzalishaji endelevu na wenye tija,” amesema Kiongozi huyo Mkuu wa Taasisi ya OSHA.
Lilian Kombe, Mfanyakazi wa Mahakama Kuu-Kanda ya Morogoro ambaye alishiriki mafunzo yalitolewa na Wakaguzi wa OSHA mara baada ya kuhitimisha ukaguzi wao, amesema wamejifunza mambo mengi kuhusu afya na usalama wao wanapokuwa kazini ikiwemo usalama wa mifumo ya umeme pamoja na masuala ya kiegonomia.
OSHA ni Taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) yenye jukumu la kulinda nguvukazi ya Taifa pamoja na rasilimali nyingine zilizowekezwa katika sekta ya umma na binafsi. Miongoni mwa mambo yaliyotazamwa na OSHA katika ukaguzi huo ni pamoja na usalama wa mifumo ya umeme, mashine na zana kufanyia kazi, masuala ya kiegonomia pamoja na ukaguzi wa afya na mazingira ya kazi.
0 Comments