-Gekul aagiza watuhumiwa kuchunguzwa.
Na Lusajo Mwakabuku – WKS MANYARA
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul ameuagiza Uongozi wa Ofisi ya Mashtaka Mkoa wa Manyara pamoja na viongozi wa Jeshi la Polisi Mkoani humo kufanya uchunguzi juu ya tuhuma zilizotolewa na mahabusu na Wafungwa wa gereza la Babati Mjini dhidi ya askari na watumishi wa vyombo hivyo vya haki ambapo katika nyakati tofauti wameonekana kutumia nafasi zao kudai rushwa kwa malengo ya kukwepesha haki.
Tuhuma hizo zimetolewa tarehe 24/05/2023 wakati timu ya wataalam wanaoendesha Mama Samia Legal Aid Campaign ikiongozwa na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul ilipofika gerezani hapo kwa lengo la kutoa elimu pamoja na msaada wa kisheria kwa wafungwa na mahabusu ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa kampeni hiyo kubwa iliyozinduliwa mwanzoni mwa mwaka huu ambayo itadumu kwa miaka mitatu mpaka 2026.
Akiambatana na wataalamu kutoka Ofisi ya Mashtaka, Tume ya haki za binadamu, Mrakibu wa Polisi wa Mkoa, Dawati la jinsia la polisi, Wanasheria na watumishi wengine kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Naibu Waziri Gekul alifika katika gereza la Babati na kufanikiwa kuongea na uongozi lakini pia na wafungwa na mahabusu waliokuwepo katika gereza hilo lengo likiwa ni kubaini changamoto za kisheria zikiwemo upatikanaji wa dhamana kwa wafungwa wanaostahili pamoja na namna kesi zao zinavyoendeshwa.
Timu ya wataalam wa Mama Samia Legal Aid Campaign ilipokewa na uongozi wa Gereza hilo ambapo pamoja na mambo mengine, Kamishna Msaidizi wa Magereza ACP Nkonge Edwin alimweleza Naibu Waziri kuwa moja kati ya vitu ambavyo gereza hilo limefanikiwa kuvitekeleza ni pamoja na kesi kusikilizwa kwa wakati kitu ambacho ni kilio kwa watu wengi walio vizuizini katika maeneo mengine huku akiainisha kasoro ndogondogo zikiwemo uchakavu wa vyombo vya usafiri katika kutoa huduma za wafungwa pamoja na kukataliwa kwa rufani zilizo nje ya muda.
Timu hiyo ya Mama Samia Legal Aid Campaign baada ya kuongea na uongozi wa Gereza iliingia ndani ya gereza na kuongeza na mahabusu pamoja na wafungwa ambapo elimu ya sheria ilitolewa jinsi mtu anavyokamatwa kituoni mpaka anapelekwa gerezani vitu vinavyotakiwa kufuatwa, Lakini pia mtaalam kutoka haki za binadamu alielezea haki za msingi za wafungwa wakiwemo gerezani ikiwemo haki ya dhamana kwa makosa yenye dhamana na pia Ofisa kutoka Ofisi ya Mashtaka akaongelea wajibu wa Ofisa wa mashtaka wa wilaya na muda uliopangwa kisheria wa kushughulikia kesi za watu walio vizuizini ambapo kwa kwa mkoa huu hali imeonekana kuwa shwari kwani hakuna mfungwa au maabusu aliyelalamika kupitilizwa muda wa siku 90 wa kusomewa shitaka lake mara wanapowekwa vizuizini kwa mujibu wa sheria.
Ilipofika wakati wa maswali, wafungwa na mahabusu walianza kwa kubainisha changamoto zao wanazokumbana nazo kupitia risala iliyosomwa na Mahabusu Michael Marko ambayo pamoja na mengine ilielezea changamoto ya ucheleweshaji wa upelelezi wa kesi unakopelekea mrudikano wa mahabusu gerezani, Ucheleweshwaji wan akala za hukumu kwa watu ambao wameshahukumiwa, Kuporwa fedha wakati wakikamatwa na polisi na pia wakasema kumekuwa na kawaida ya mahabusu kukamatwa na kuachiwa huku pia wakiituhumu Ofisi ya Mashtaka kutokuleta mashahidi kwa wakati.
Hali ikazidi kubadilika mara baada ya wafungwa na mahabusu hao kupewa nafasi ambapo bila kusita wala uoga waliwataja maaskali na maofisa upelelezi pamoja na makarani wa mahakama kwa majina ambao waliwapora fedha wakati wakikamatwa na wengine kuwataka walipe ili kesi zao zisiendelee. Na pia mahabusu na wafungwa hao walieleza kuwa walitakiwa kutoa hela zilizoanzia milioni mbili na kuendelea ili waachiwe wakati mahabusu mwingine akidai askari alimwambia mke wake atoke Singida aje alale Manyara na siku ya pili mumewe ataachiwa (Akiashiria rushwa ya ngono)
Baada ya kupokea malalamiko hayo, Naibu Waziri aliwaagiza viongozi wa polisi pamoja na wa Ofisi ya Mashtaka alioambatana nao kuhakikisha kuwa wale wote waliotajwa katika tuhuma hizo uchunguzi wa kina unafanyika na wale wote watakaobainika kuwa wametumia mamlaka yaka yao vibaya basi hatua kali za sheria zichukuliwe dhidi yao na pia akawaagiza viongozi ha kuhakikisha wana jitihada za upatikanaji wa haki kwa mahabusu na wafungwa hao unapatika kwa wakati na bila usumbufu.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul akifuatilia kwa makini taarifa inayotolewa na Kamishna Msaidizi wa Magereza ACP Nkonge Edwin alipofika gerezani hapo na timu ya wataalam wa Mama Samia Legal Aid Campaign.
Kamishna Msaidizi wa Magereza ACP Nkonge Edwin akisoma taarifa ya Gereza la Babati mara baada ya Mhe. Gekul na timu yake kuwasili katika gereza hilo kwa lengo la kutoa elimu na msaada wa kisheria.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul akisikiliza kesi ya mahabusu Mwajuma Mada aliyefika gerezani hapo ikiwa ni sehemu ya msaada unaotolewa na timu hiyo kwa watu walio vizuizini
.Timu ya wataalamu na uongozi wa gereza wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumaliza kazi hiyo ya kutoa msaada wa kisheria kwa watu walio vizuizini.
0 Comments