Ticker

6/recent/ticker-posts

RAIS SAMIA APONGEZWA KUUPA HESHIMA MKOA WA SINGIDA KUSIMAMIA MAADHIMISHO YA SIKU YA NYUKI DUNIANI


Na Mwandishi wetu Singida,

Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Mragiri amempongeza Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuupa heshima Mkoa huo kusimamia maonesho ya kitaifa ya Maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani yaliyoanza Mei 18 hadi 21, 2023.

Mragiri amezungumza hayo leo akiwa katika Kijiji cha Kitaraka wilaya ya Manyoni mkoani humo yanapofanyika Maadhimisho hayo kwenye viwanja vya Bombadia.

"Hii ni Heshima kubwa ambayo tumepewa , lakini tumepewa heshima hii Wakazi wa Singida kwa kuwa ni mkoa unaozalisha sana mazao ya nyuki" amesema.

Aidha , amesema kupitia maonesho hayo wananchi wanazidi kumiminika katika viwanja hivyo kujionea fursa na bidhaa mbalimbali zinazotokana na mazao ya nyuki.

"Watu wengi walikuwa wanajua nyuki alikuwa anatoa zao moja la asali, lakini kumbe kuna mazao mengi ambayo yana faida sana . " ameongeza.

Wakati huo huo, amewataka wananchi wa mkoa huo kuchangamkia fursa ya ufugaji nyuki , kwani imekuwa ni chanzo kizuri cha kipato kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

"Vipo vikundi vinajipatia fedha kutokana na zao hili la ufugaji nyuki. Tunapofanya ufugaji nyuki tunaimarisha kizazi cha nyuki kisipotee duniani" amesisitiza.

Sanjari na hayo , amesema wakazi wa Singida wanapaswa kutunza misitu ambayo itasaidia kujiendeleza kiuchumi kupitia zao la nyuki.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, Deusdedith Bwoyo amesema ni wakati sasa kwa Watanzania kuweka mkazo katika biashara ya ufugaji nyuki huku akiwaasa Watanzania kutumia fursa hiyo kufuga kibiashara

" Ni wakati sasa inabidi tuache kufuga nyuki kizamani, tufuge Nyuki kibiashara." amesema.

Post a Comment

0 Comments