Ticker

6/recent/ticker-posts

TBS KANDA YA MAGHARIBI YATOA ELIMU KWA WAFANYABIASHARA WA VIPODOZI MIKOA YA RUKWA,KATAVI,KIGOMA


Kaimu Meneja wa Kanda ya Magharibi (TBS) Bw.Rodney Alananga akiongea na wafanyabiashara wa Vipodozi wa mkoa wa Kigoma wakati wa mafunzo Hayo yaliyofanyika mapema leo


*************

Na Mwandishi Wetu, Kigoma

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Magharibi limetoa elimu kwa wafanyabiashara wa vipodozi kwenye mikoa mitatu ya Kigoma, Rukwa na Katavi ili waweze kuuza Vipodozi vilivyokidhi vigezo kwa mujibu na taratibu za kisheria.

Elimu hiyo inalenga kuwawezesha kuingiza na kuuza bidhaa za vipodozi vilivyoruhusiwa nchini ili kulinda afya za Watanzania ambao ndio wateja wao wa kila siku.

Kaimu Meneja wa TBS Kanda ya Magharibi, Rodney Alananga, kupitia taarifa yake ya kuhitimisha program ya utoaji elimu kwa wadau wa vipodozi iliyofanyia kuanzia Mei 10 hadi 18 Mwaka Huu, alisema wasipofuata taratibu itawapelekea kupata hasara mara kwa mara kwa kukamata bidhaa zao, kulipa faini na gharama za uteketezaji vitu ambavyo hudidimiza mitaji ya biashara zao.".

"Tunatoa Rai pia kwa Wasafirishaji wa abiria magari madogo na makubwa wenye mabasi wasitumike kubeba bidhaa zisizokidhi viwango wanaouza katika mabasi ya abiria waache mara moja," alisema Alananga na kusisitiza;

“ Kwa wafanyabiashara lazima wazingatie taratibu za kisheria walizofundishwa ili waingize na kuuza bidhaa za vipodozi vilivyoruhusiwa tu ili kulinda afya za Watanzania ."

Kuhusu maoni na mapendekezo yaliyotolewa na wadau, Alananga alisema yamepokelewa na yatafanyiwa kazi.

Miongoni mwa maoni na mapendekezo hayo ni kuiomba TBS iongeze juhudi ya udhibiti katika soko kwa kutoa elimu zaidi, kufanya ukaguzi mipakani hasa bandari ya Dar es Salaam na kwa wauzaji katika mkoa husika.

"Hivyo, TBS itaendelea kutoa elimu lakini pia kufanya kaguzi duka kwa duka na mipaka yote na kuchukua hatua kali za kisheria kwa watakaobainika kukutwa wakiuza na kusambaza vipodozi vyenye viambata sumu ," alisema.

Alisema TBS ndiyo yenye dhamana ya kusimamia ubora na usalama wa vipodozi vinavyoingia kutoka nje ya nchi na vinavyozalishwa nchini.

Baadhi ya washiriki mkoani Rukwa
Washiriki wilayani Kasulu Mkoani Kigoma

Baadhi wa washiriki wa elimu ya Vipodozi manispaa ya Mpanda mkoani Katavi

Post a Comment

0 Comments