Kufanya biashara ya kimataifa na kufikia masoko ya bidhaa za thamani ya juu, wazalishaji lazima waweze kuonyesha kwamba wanakidhi viwango vya chakula na zaidi ya hayo, serikali inahitaji kuhakikisha usalama na biashara ya haki hasa katika masoko ya ndani kwa ajili ya chakula.
Haya yote yanaungwa mkono na vipimo vya kuaminika na sahihi vya kiasi (quantity) na ubora (quality) wa bidhaa ghafi na zilizochakatwa.
Ameyasema hayo leo Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhandisi Emmanuela Kaganda ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Arumeru wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Vipimo Duniani yaliyofanyika Kitaifa mkoani Arusha Mei 30,2023.
Amesema Sayansi ya Vipimo ina umuhimu mkubwa katika nyanja mbalimbali za kiuchumi, nishati, viwanda, taaluma, utafiti, afya na mazingira kwani husaidia kuwa na ulinganifu wa vipimo dunaini, husaidia uzalishaji wa viwanda na husaidia pia kutathimini ubora wa bidhaa (conformity assessment).
Aidha amesema upatikanaji wa chakula salama na cha bei nafuu ni mojawapo ya changamoto kubwa kwa kila mmoja wetu na kwa serikali duniani. Hili pia ndilo lengo la wakulima na wazalishaji wa chakula ambao wanafanya biashara ya bidhaa kupitia wasambazaji na wauzaji reja reja kwa watumiaji katika ngazi za kimataifa, kitaifa na ndani.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Yusuph Ngenya amewataka watanzania kutumia bidhaa zilizothibitishwa kuwa na ubora na TBS, hii itahakikisha kuwa tunatumia bidhaa bora na salama kwa afya zetu na za familia zetu.
Hata hivyo Dkt.Ngenya amesema vipimo ni kiungo muhimu katika mnyororo mzima wa thamani, pia ni zana muhimu kuthibitisha ubora wa bidhaa kutoka alama ya ubora au usajili bidhaa
Amesema wazalishaji, wasindikaji, wasambazaji na hata watumiaji wanategemea vipimo kila siku katika mnyororo wa thamani wa chakula
"Mama nyumbani anahitaji kuhakikisha anatumia kiasi sahihi cha unga ili kupata ugali wa kutosha kwa familia yake. Muoka mikate anahitaji kupima kilakiungo anachotumia ili kuzalisha mikate bora na inayovutia wateja". Amesema
0 Comments