Ticker

6/recent/ticker-posts

WAMILIKI WA VIWANDA WATAKIWA KUTUMIA TAALUMA YA KAIZEN KUUNGA MKONO JUHUDI ZA SERIKALI



Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah amewaomba wamiliki wa viwanda kutumia taaluma ya KAIZEN kuunga mkono juhudi za Serikali kufungamanisha uchumi kupitia Sekta za Viwanda na Biashara ili kuleta matokeo chanya katika taifa.

Ameyasema hayo tarehe 12 Mei, 2022 alipokua akizungumza na wakufunzi na wenye viwanda wanaotekeleza dhana ya KAIZEN jijini Dar es salaam.

Dkt. Hashil amesema utekelezaji wa KAIZEN katika sekta ya viwanda kumewezesha kuandaliwa kwa takriban waratibu 200 wa KAIZEN kutoka viwandani, na wakufunzi wa KAIZEN 300 ambapo 175 wamepatiwa vyeti na tayari wakufunzi 84 wamesajiliwa.

“Inatarajiwa kuwa wakufunzi wote waliopo wanaendelea kutoa mafunzo ya KAIZEN viwandani ili kuongeza tija na kuongeza thamani katika mnyororo wa thamani".

Amesema lengo ni kuyafikia maeneo mengi kisekta kwa haraka, mijini na vijijini. Aliongeza hadi sasa, zaidi ya viwanda 135 vimenufaika na mafunzo ya KAIZEN (vikubwa 25% na vidogo 75%).

Kwa mujibu wa Dkt. Hashil utafiti uliofanyika mwaka 2019 unaonesha kuwa kati ya viwanda 52 vilivyofanyiwa tathmini, asilimia 58 ya viwanda hivyo vilithibitisha kuwepo na mabadiliko chanya baada ya kutekeleza falsafa ya KAIZEN.

Kwa upande wake Balozi wa Japani nchini Tanzania Mhe. Yasushi Misawa amekipongeza kiwanda cha A-Z kilichopo mkoani Arusha kwa kutekeleza dhana ya KAIZEN na kuibuka mshindi katika mashindano ya KAIZEN Africa yaliyofanyika nchini Tunisia.

“Nimevutiwa na namna dhana ya KAIZEN ilivyoenea nchini Tanzania na nilitembelea kiwanda cha A-Z na kujionea kwa namna gani KAIZEN inasaidia kuleta uzalishaji wenye tija na ubora katika kiwanda” alisema.

Mwakilishi Mkuu wa JICA, ARA Hitoshi amesema shirika hilo limeandaa mradi mpya wa kuimarisha viwanda kupitia huduma za maendeleo ya biashara na uongezaji wa tija na ubora viwandani KAIZEN.

“ Mradi huu hautoangalia utekelezaji wa KAIZEN peke yake, lakini pia huduma za maendeleo ya biashara kama masoko, masoko, mikakati ya biashara, uhasibu, pamoja na rasilimali watu.

Aliongeza kuwa mradi huo utajumuisha Zanzibar na mikao nane ya Tanzania Bara ikiwemo Dar es salaam, Arusha, Kilimanjaro, Mwanza,Mbeya, Dodoma, Singida na Morogoro.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo Cha Biashara (CBE) Prof. Edda Lwoga amesema chuo kimeendelea kuandaa wakufunzi wa KAIZEN ambapo mwaka 2022 jumla ya wakufunzi 65 na waratibu 33 walizalishwa katika mikoa ya Mtwara, Pwani, Kagera na Tanga.

“Baadhi ya dhana na misingi ya KAIZEN imejumuishwa katika mitaala ya kufundishia chuoni, mfano mbinu za 5S KAIZEN zimejumuishwa katika mtaala wa utunzaji wa ofisi na nyaraka”.

Aidha amesema wameendelea kutoa mafunzo ya KAIZEN na mbinu za kibiashara kwa wajasiriamali wadogo na vikundi ama wanachama wa vikoba ili waweze kuzalisha kwa tija na Ubora.

KAIZEN ni neno la Kijapani lenye maana ya mabadiliko endelevu mazuri kuelekea kwenye ukuaji wa uchumi ambayo huratibiwa na Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kupitia Kitengo cha KAIZEN na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japani (JICA).

Post a Comment

0 Comments