Ticker

6/recent/ticker-posts

MKUTANO WA MAJADILIANO WA MASUALA YA UJUZI NA WADAU WA CHAMA CHA WAAJIRI TANZANIA WAFANYIKA JIJINI DAR ES SALAAM

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulamavu kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali katika program ya kukuza ujuzi , mpaka sasa Vijana wapatao 91,106 wamenufaika na mafunzo ya Uanagenzi.

Ameyasema hayo leo Juni 22,2023 Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira Na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi Katika Mkutano wa Majadiliano wa Masuala ya Ujuzi na Wadau wa Chama Cha Waajiri Tanzania Jijini Dar es Salaam.

Amesema Vijana wapatao 22,296 wamenufaika na mafunzo ya urasimishaji ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu (RPL) na vilevile Vijana wapatao 6,300 wamenufaika na mafunzo ya uzoefu wa kazi kwa wanaohitimu vyuo vya elimu ya juu na ya kati na Vijana 2,196 wamenufaika na mafunzo ya kukuza ujuzi kwa walio makazini kwa sekta ya umma na binafsi.

Aidha amewapongeza ATE kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele katika masuala mbalimbali ikiwemo ya kuhamasisha Usawa wa Kijinsia katika maeneo ya kazi hasa kupitia utekelezaji wa Programu ya Mwanamke Kiongozi inayolenga kuwajengea uwezo Wanawake kushika nafasi za Juu za Uongozi.

"Jumla ya Wanawake 274 Pamoja na Wabunge Wanawake wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Wajumbe Wanawake wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar 150 wameshapatiwa mafunzo haya". Amesema

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa ATE, Bi.Suzanne Ndomba amesema kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi, Serikali imetoa fursa za mafunzo ya ujuzi wa kujiajiri au kuajiriwa kwa vijana 14,542 mbalimbali kupitia mafunzo ya uanagenzi na uzoefu kazini.

Bi.Suzanne ameipongeza Serikali kwa kuendelea kutoa hamasa kupitia Sera na Mipango mbalimbali ili kuchochea ushiriki wa waajiri katika kuendeleza ujuzi lakini pia katika kutengeneza fursa za ajira hapa nchini.

"Tumeshuhudia katika hotuba ya Bajeti Kuu ya nchi ya mwaka wa fedha 2023/24 iliyowasilishwa Bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango, Mh. Dr. Mwigulu Lameck Nchemba (MB) na sasa katika Finance Bill ya Mwaka 2023 ambapo imependekezwa Tozo ya Kuendeleza Ujuzi (SDL) ishuke kutoka asilimia 4 hadi 3.5 na kuahidi kuendelea kuishusha taratibu kwa lengo la kupunguza gharama za kuajiri na kuchochea fursa za ajira nchini bila kuathiri kwa kiasi kikubwa mapato ya Serikali na mipango yake". Ameeleza Bi.Suzanne.
Afisa Mtendaji Mkuu wa ATE, Bi.Suzanne Ndomba akizungumza katika Mkutano wa Majadiliano wa Masuala ya Ujuzi na Wadau wa Chama Cha Waajiri Tanzania leo Juni 22,2023 Jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira Na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi akizungumza katika Mkutano wa Majadiliano wa Masuala ya Ujuzi na Wadau wa Chama Cha Waajiri Tanzania leo Juni 22,2023 Jijini Dar es Salaam.
Wadau mbalimbali wakiwa katika Mkutano wa Majadiliano wa Masuala ya Ujuzi na Wadau wa Chama Cha Waajiri Tanzania leo Juni 22,2023 Jijini Dar es Salaam.



Post a Comment

0 Comments