WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amewataka wawekezaji wa migodi nchini kuhakikisha wanapofanya shughuli za uchimbaji madini wanarejesha maeneo hayo ili kuhakikisha mazingira yanakuwa salama na kuimarisha ikolojia.
Ametoa maagizo hayo leo Juni 21,2023 wakati alipofanya ziara ya kutembelea maeneo ya uwekezaji katika upande wa Makaa ya Mawe mkoani Ruvuma.
Aidha amewapongeza wawekezaji wa migodi mkoani Ruvuma kwa kuhakikisha maeneo ambayo wanachimba Makaa ya Mawe wwanakarabati na kurrejesha udongo katika maeneo hayo.
Pamoja na hayo amemuelekeza Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuhakikisha anatembelea migodi hasa iliyopo Kanda ya Ziwa na kuhakikisha anatoa maelekezo ya haraka ili migodi hiyo kufanya urejeshaji wa ardhi iliyoharibiwa.
Hata hivyo ametoa maelekezo migodi hiyo kuhakikisha katika maeneo yao wanadhibiti utiririkaji wa maji ambayo inawezekana yakawa na athari kwa maisha ya watu kutokana na tindikali inayozalishwa Salfa ambayo inaambatana na uchimbaji wa Makaa ya Mawe
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samuel Gwamaka amesema kuwa atahakikisha anashirikiana bega kwa bega na sekta zote za uchimbaji wa rasilimali madini katika utunzaji wa mazingira kwenye maeneo hayo.Na pia ameagiza migodi yote kuandaa Mipango ya Ukarabati wa Mazingira na kuwasilisha NEMC.
"Katika ziara tulioifanya, sehemu kubwa ya masharti ya vyeti vya mazingira yanafuatwa karibu kampuni zote tulizotembelea, hilo linatia moyo lakini bado kuna maeneo machache ambayo tunapenda waendelee kuyafanyia kazi kubwa". Amesema Dkt. Gwamaka
Kwa upande wa Wasimamizi wa Mazingira kwenye migodi hiyo,wameahidi kuyashughulikia maelekezo yote yaliyotolewa na kuhakikisha wanatunza mazingira katika zoezi la uchimbaji wa Makaa ya Mawe.
0 Comments