Na John Mapepele - Mbarali
Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inakwenda kurejesha hekta 74,432 kwa wananchi wa Mbarali zilizokuwa Eneo la Hifadhi ya Taifa ya Ruaha baada ya zoezi hilo la kuziomba kushindikana kwa takribani miaka saba ili zitumike katika shughuli mbalimbali za kibinadamu ikiwa ni pamoja na ufugaji na kilimo.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa katika kikao cha pamoja baina Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Wabunge wa Mbarali, Uongozi wa CCM wilaya ya Mbarali na Uongozi wa Hifadhi za Taifa (TANAPA) kilichofanyika eneo la Kapunga kata ya Itamboleo wilayani Mbarali na baadaye kuelekea kwenye maeneo ya mipaka yenye migogoro na kuongea na wananchi wa maeneo hayo Juni 22 mwaka huu.
Mhe. Mchengerwa amesema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa migogoro yote ya mipaka inamalizika kwa haraka ili lengo la kuhifadhi raslimali maeneo hayo na raslimali za taifa na kuboresha maisha ya wananchi yanafikiwa.
Amesema katika kipindi hiki kifupi cha Serikali ya mama Samia tayari maeneo mengi yameshafikiwa na kutatua migogoro ya mipaka iliyodumu kwa muda mrefu ikiwa ni pamoja na eneo vijiji vya Tarime vinavyozunguka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambapo amewaomba wananchi kuwa watulivu na kushirikiana na Serikali yao katika kutatua migogoro hiyo kwa kuwa hakuna jambo linaloshindikana.
Aidha, amewaomba wananchi kutambua kuwa maeneo yaliyotengwa kwa uhifadhi yana umuhimu mkubwa kwa shughuli mbalimbali za kimaendeleo kwa kuwa ndiyo vyanzo vya maji yanayokwenda kwenye bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere ambalo ndilo chanzo kikuu cha uzalishali wa umeme kwa taifa letu.
Akiwapitisha kwenye andiko la tathmini ya eneo hilo Mjumbe wa Kamati ya Mkoa wa Mbeya ya kufanya tathmini ya utekelezaji wa uwekaji wa mpaka unaoendelea katika wilaya za Mbarali na Chunya mkoani Mbeya Kamishna Msaidizi wa Mkoa wa Mbeya Syabumi Mwaipopo ameiambia kamati na viongozi wote waliofika katika kikao hicho kuwa kamati ilizingatia mambo mbalimbali wakati wa kufanya tathmini hiyo ili iwe na gtija na iendane na uhalisia.
Ameyajata baadhi ya mambo yaliyozingatiwa kuwa ni pamoja na mwinuko kutoka usawa wa bahari, uoto wa mimea, uwepo wa ardhi oevu na shughuli za kibinadamu zenye athari za kimazingira ambapo pia alisema mapendekezo ya maboresho ya GN 28 yalikuwa ni shamba la madibila phase 2 libaki katika hifadhi wakati Madibila phase 1 liachwe huru kwa wananchi, eneo la NARCO litolewe ndani ya Hifadhi na vijiji vitano pekee badala ya kumi na sita vya awali wapishe hifadhi.
Akizungumzia kuhusu madai yay a Shamba la Kapunga kutopitiwa na mipaka mipya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Juma Homera amefafanua kuwa shamba hili halikupitiwa na GN 28 mpya kwa sababu GN mpya inapita katika maeneo yale yale yaliyopitiwa na GN.28 na wala haianzishi maeneo mapya ambayo hata ile ya awali haikupitiwa.
Hata, hivyo wananchi watambue kuwa Kapunga Estate ni shamba la serikali na huyu mwekezaji amepewa awekeze tu kwa muda maalum, na mkataba wake utakapoisha shamba hili litarudi serikalini.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe.Timotheo Paul Mnzava alisema kamati hii ya Bunge inasimamia shughuli za Maliasili na Ardhi kwa niaba ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivyo basi msingi wa safari hiyo ni kujiridhisha ili kulishauri Bunge kuona namna bora kumaliza hili jambo.
Aidha, mwenyekiti huyo aliongeza kuwa nchi ni yetu sote lazima tulinde wananchi wetu na pia tulinde Maliasili zetu kwa ajili ya kizazi cha sasa na kizazi kijacho.
Amesema kuwa baada ya kamati hii kutembelea uwandani na kujionea hali halisi itawasilisha mapendekezo ya walichokiona bungeni ili kubadili GN.28 na kuja na GN. mpya ambayo itakuwa ni suluhu kwa mgogoro uliodumu zaidi ya miaka 18.
0 Comments