Na Mwandishi Wetu, Katavi
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imefanya jitihada mbalimbali za kufanya vikao na wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara kutoka nchi jirani ambazo zinatumia bandari ya kimkakati ya Karema.
Lengo la kufanyika kwa vikao hivyo ni kuendeleza ushirikiano wa kibiashara kwa kuitumia bandari hii ombi ambao lilikubaliwa likiambatana na changamoto walizowasilisha wadau hao.
Meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika Edward Mabula amewaambia waandishi wa habari kwamba vikao vya wadau vimehusisha pia nchi za Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Burundi na hiyo imelenga kuhakikisha bandari ya kimkakati ya Karema iliyopo wilayani Tanganyika mkoani Katavi inafanya kazi vizuri zaidi na kuongeza mapato,
Akielezea zaidi kuhusu bandari hiyo amesema pamoja na uwepo wa changamoto ya miundombinu ya barabara kuwa mibovu,imeweza kuhudumia tani 4,500 ya shehena ya mzigo mbalimbali na abiria 2970 hadi kufikia mwezi Mei, mwaka huu.
Aidha amesema Serikali imeshaanza kutekeleza mikakati ya kuongeza uwezo wa kutoa huduma bandari za ziwa Tanganyika ikiwemo Karema kwa kuanza ujenzi wa meli mbili kubwa za kisasa na kutangaza zabuni ya ujenzi wa barabara ya kuelekea katika bandari ya Karema.
Pia amesema tayari kuna ahadi ya Serikali ya kujenga meli mbili kubwa, moja yenye uwezo wa kubeba mizigo hadi tani 3,000 na nyingine yenye uwezo kuchukua abiria 400 na tani 600 za mizigo, tayari ujenzi wa meli hizi umeshaanza.
Kuhusu changamoto ya ubovu wa barabara kuelekea katika bandari Karema tayari imetangazwa katika gazeti la serikali na taratibu za kumpata mkandarsi zinaendelea baada kuwa muda wa zabuni kukamilika mwisho wa Mei, mwaka huu.
"Nitumie fursa hii kuikaribisha sekta binafsi kuwekeza katika bandari ya Karema kupitia fursa mbalimbali zinazotokana na bandari hiyo ikiwemo kuwekeza katika vyombo vya usafiri kama vile meli na boti."
Kwa upande wake Nahodha wa boti inayofanya shughuli za usafiri na usafirishaji kati ya nchi ya Tanzania na Jamhuri ya Muungano wa , Amos Kapena amesema kutokana na maboresho yaliyofanywa katika bandari hiyo yamepunguza gharama na hasara kwa mteja na wamiliki wa vyombo.
"Hasara na gharama hizo zilitokana na kushindwa kwa meli au boti kupakuliwa bandarini na hivyo kutumia mitumbwi kupakua mizigo na kuufikisha katika bandari, " amesema.
Wakati huo huo mmoja wa wananchi wa Karema ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi wilaya ya Tanganyika, Joseph Edward amesema ujio wa bandari ya Karema umeleta manufaa lukuki kwa wakazi wa Karema, wilaya ya Tanganyika, Mkoa wa Katavi na Taifa kwa ujumla.
Hata hivyo waandishi waliotembelea bandari hiyo wameelezwa bandari ya Karema ipo umbali wa kilomita 123 kutoka Mpanda ambapo ujenzi wake ulianza mwaka 2019 kwa gharama ya Sh.Bilioni 47.9 ambapo sasa inatajwa na wafanyabiashara kama mkombozi wa uchumi wao kwa kusafirisha bidhaa zao kutoka Tanzania kwenda nchi jirani.
Meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika, Edward Mabula akitoa taarifa ya utendaji kazi wa bandari ya Karema kwa waandishi wa habari waliotembelea bandari hiyo Juni 03, 2023.
Mwananchi na mkazi wa Karema, Joseph Edward akiongelea na wananchi walivyonufaika na uwepo wa bandari hiyo
Nahodha Almas Kapena akielezea kuhusu huduma zinazotolewa sasa hususan za kupakia na kupakua mizigo namna zilizovyoboreshwa katika bandari ya Karema
Mwonekano wa miundombinu mbalimbali katika bandari ya Karema
0 Comments