Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Mcha Hassan Mcha na Mkurugenzi Mtendaji Huduma za Shirika wa Mamlaka ya Mapato Malawi (MRA) Bi. Agnes Katsonga Phiri wamezindua mfumo wa kubadilishana taarifa kwa njia ya kielektroniki.
Hafla ya uzinduzi huo imefanyika katika kituo cha Forodha cha Pamoja (OSBP) Kasumulu kilichopo katika Wilaya ya Kyela Mkoani Mbeya.
Akizungumza wakati wa uzinduzi Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Mcha Hassan amesema mfumo huo utasaidia kuokoa muda na gharama pia kuongeza ufanisi wa biashara ya mipakani na kuchochea ukuaji wa uchumi wa kikanda.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Huduma za Shirika wa Mamlaka ya Mapato Malawi (MRA) Bi. Agnes Katsonga Phiri amesema mfumo huu unalenga kurahisisha michakato ya forodha, kukuza uwazi, na kuwezesha shughuli za biashara. Kuunganishwa kwa TRA-TANCIS na MRA ASYCUDA World kutaleta mapinduzi katika michakato ya kibali, kunufaisha wafanyabiashara na watu binafsi nchini Tanzania na Malawi" amesema.
Mradi huu umefadhiriwa na Umoja wa Watu wa Wingereza kupitia Trademark Africa. Mwakilishi wa wafadhiri hao ambaye ni Mkurugenzi wa Nchi wa Trademark Africa, Dr. Jovin Mwemezi amepongeza umuhimu na manufaa ya mradi huo akisema, “Tunafuraha kuunga mkono mradi huu wa msingi utakaoleta mapinduzi ya biashara ya mipakani kati ya Malawi and Tanzania.
Aidha Wasafirishaji wa mizigo wamepongeza jitihada hizo kwani kubadilishana taarifa kwa njia ya kielekroniki ni muhimu kwa tasnia ya usafirishaji wa mizigo baina ya Nchi na Nchi kwani unawezesha kutoa huduma za haraka, zenye ufanisi zaidi kwa wateja, kuongeza ushindani wa biashara na kukuza biashara ya kimataifa.
0 Comments