Ticker

6/recent/ticker-posts

WATENDAJI VITUO VYA HUDUMA ZA AFYA DAR WATAKIWA KUWA NA TAKWIMU NA MAOTEO SAHIHI NA KUYAPELEKA MSD KWA WAKATI

Na Said Mwishehe

KATIBU Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam Rehema Madenge ametoa mwito kwa watendaji wote wa vituo vya kutolea huduma za afya kuwa na takwimu na maoteo sahihi na kuyapeleka kwa Bohari ya Dawa(MSD) ili waweze kupata bidhaa za afya kwa wakati kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.

Madenge ametoa mwito huo leo Juni 27,2023 wakati wa kikao kazi kilichooitishwa na Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Dar es Salaam na kuwahusisha wadau mbalimbali wakiwemo watendaji wa sekta ya afya kwa mamlaka za Serikali za Mtaa kwa mkoa wa Dar es Salaam.

“Tuko Bohari ya Dawa MSD)kwa ajili ya kikao kazi kinajumuisha watendaji kutoka katika sekta ya afya kwa mamlaka zetu za serikali za mtaa kwa mkoa wa Dar es Salaam na tumekuja kwa ajili ya kujadiliana lakini kupata uzoefu na kujifunza mashirikiano na wenzetu wa MSD kutokana na suala zima la upatikanaji wa bidhaa za afya katika vituo vyetu vya kutolea huduma.

“Serikali imefanya kazi kubwa sana ya kuboresha vituo vya kutolea huduma za afya nchi nzima , ambayo maana yake ni nini?Maana yake ni kwamba wanataraji wananchi wetu wakapate huduma bora za afya kwenye vituo vyetu vya kutolea huduma.

“Lakini hilo haliwezi kuwa endapo hatutakuwa na bidhaa za afya katika vituo vyetu na ili tuwe na biadhaa za afya inahitaji pande zote mbili kwa maana kwetu sisi watendaji kwenye vituo vya kutolea huduma za afya , tupeleke mahitaji yetu mapema , kwa wakati sahihi ili MSD nao watuletee bidhaa kwa wakati sahihi ndipo wananchi wetu wanaweza kupata huduma kwa wakati,”amesema.

Hivyo amesema ili kufanikisha utoaji huduma za bidhaa za afya kwa wakati lazima watendaji wa vituo vya kutolea huduma za afya wawe na takwimu sahihi , maoteo sahihi yatakayoonesha mahitaji sahihi na kisha kupeleka kwa wakati MSD

“Pia kuna suala zima la ukusanyaji mapato kwenye vituo vyetu vya kutolea huduma wanastahili kukusanya mapato yale vizuri kwa usahihi lakini wajaze fomu za bima kwa usahihi ili kusudi fedha ipatikane ambayo itasaidia katika kulipia bidhaa hizo ambazo wanazinunua kutoka MSD.

“Lakini wenzetu wa MSD nao watakapopata maoteo yetu kwa wakati nao watupatie huduma kwa maana ya vifaa tiba, dawa na vitendanishi kwa wakati ambayo inategemea wananchi wetu kupata huduma kwa wakati .Kwa hiyo inahitajika mawasiliano ya mara kwa mara baina yetu ili yatusaidie wananchi kupata huduma kwa wakati.”

Aidha ametumia nafasi hiyo kuipongeza MSD kwa kazi kubwa na nzuri wanayofanya katika kuhakikisha bidhaa za afya zinapatikana wakati wote huku pia akipongeza hatua ya MSD kuwa na viwanda vyake vya kutengeneza vifaa tiba zikiwemo barakoa za N-95.

Kwa upande wake Meneja wa MSD Kanda ya Dar es Salaam Betie Kaema ametumia nafasi hiyo kufafanua kuwa kanda hiyo ni miongoni mwa kanda 10 za bohari hiyo nchini ambayo inahudumia wateja wa bidhaa za afya.

“Kanda ya Dar es Salaam inahudumia mikoa minne ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro pamoja na Zanzibar. Leo ni siku ambayo Kanda ya Dar es Salaam MSD tumekutana na wadau wetu kwani tunao Wafamasia, watalaamu wa maabara pamoja na viongozi wa sekta ya afya katika kada mbalimbali.

“Hiki kikao si cha kwanza katika bohari yetu ya dawa ni vikao endelevu na kwa mwaka huu tumeona ya kwamba tukutane na wadau wa kanda ya Dar es Salaam na nia yetu ni kama mnavyofahamu wao ndio watumiaji wakubwa wa huduma zetu za afya zinazotolewa na MSD.

“Hivyo ni vema tukakutana nao kwa ajili ya kupata mrejesho ya namna gani wanapokea huduma zetu na kupitia kwao ndipo MSD Kanda ya Dar es Salaam tunaweza kufanya vizuri kwasababu wana mengi ya kutueleza,”amesema Kaema.

Aidha amesema kupitia kikao hicho kama kuna jambo lolote ambalo wadau wanapenda liboreshwe basi kupitia kwao huduma za MSD zitaboreshwa, hivyo kikao hicho ni muhimu na huwa wanavifanya mara kwa mara ili kupata mrejesho kuhusu utoaji huduma za afya.

Pia amesema pamoja na mambo mengine kupitia wadau hao watatoka na maazimio ya namna gani wanakwenda katika mwaka ujao huku akisisitiza wadau hao wataelezea kile ambacho MSD inatamani ili kuboresha huduma za bidhaa za afya.

“Ujumbe wetu kwa wadau wetu ni kwamba kuna maboresho mengi yanayoendelea kufanyika ndani ya MSD, yapo mengi yamefanyika na yanaendelea kufanyika na kupitia kikao hiki wadau watapokea mikakati yetu ili kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za afya unakuwa wenye kukidhi mahitaji, wategemee mikakati ambayo tutaiwasilisha kwao ndio tunakwenda kuifanyia kazi.”


Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam Rehema Madenge(aliyesimama) akizungumza leo Juni 27, 2023 wakati wa kikao cha wadau wa Bohari ya Dawa( MSD)Kanda ya Dar es Salaam


Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dk.Rashid Mfaume akizungumza wakati wa kikao kilichohusisha wadau wa MSD kanda ya Dar es Salaam kilichofanyika leo jijini Dar es Salaam


Meneja wa MSD Kanda ya Dar es Salaam Betie Kaema( wa kwanza kulia) akiandika maelezo yaliyokuwa yakitolewa na wadau wakati wa kikao kazi kilichofanyika leo Juni 27, 2023.




Kaimu Mkurugenzi wa Leopold Shayo (kushoto) Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam Rehema Madenge( wa pili kushoto) Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dk.Rashid Mfaume( wa tatu kushoto) pamoja na Meneja wa MSD Kanda ya Dar es Salaam( wa kwanza kulia) wakiwa katika kikao cha wadau wa bohari hiyo kilichofanyika leo jijini
Mmoja wa watumishi wa Bohari ya Dawa( MSD) akielezea kuhusu uzalishaji wa barakoa za N95 kwa viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiongozwa na Katibu Tawala wa mkoa huo Rehema Madenge ( wa pili kushoto) walipotembelea kiwanda cha kuzalisha barako kabla ya kuanza kwa kikao cha wadau wa bohari hiyo
Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam Rehema Madenge( kulia) akijadiliana jambo na Meneja wa MSD Kanda ya Dar es Salaam Betie Kaema ( kulia) baada ya kutembelea moja ya maghala ya kuhifadhia bidhaa za afya baada ya kutembelea bohari hiyo
Sehemu ya wadau wa Bohari ya MSD Kanda ya Dar es Salaam wakiwa kwenye kikao kazi
Mmoja ya mtambo wa kutengeneza barakoa za N95 ambao uko katika Bohari ya Dawa( MSD) jijini Dar es Salaam kama unavyoonekana
Mmoja ya wafanyakazi wa kiwanda cha kutengeneza Barakoa kilichoko Bohari ya Dawa( MSD)jijini Dar es Salaam akiendelea na majukumu yake
Mkuu wa Idara ya Mawasiliano MSD Eti Kusiluka akielezea jambo wakati wa kikao kazi hicho

Post a Comment

0 Comments