Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZABUNI WATAKIWA KUZINGATIA SHERIA KATIKA MICHAKATO YA UNUNUZI.

Na Mwandishi Wetu

Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Ukidhi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma, Mhandisi Awadhi Suluo, amewataka Wazabuni wanaoshiriki katika michakato ya zabuni za umma kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za ununuzi wa umma na kuwa watakaokiuka wanaweza kufungiwa kushiriki zabuni za umma. Mhandisi Suluo amesema hayo ofisini kwake jijini Dodoma leo Ijumaa Juni 9.

Akielezea hayo, Mhandisi Suluo amesema kuwa baadhi ya wazabuni ambao wamekuwa wakipata tuzo za zabuni za umma wamekuwa wakishindwa kutekeleza matakwa ya mikataba wanayoingia na taasisi za umma na wakati mwingine kushindwa kutokea wakati wa ufungaji wa mikataba yao. Vile vile, wazabuni wengine wamekuwa wakishindwa kutekeleza mikataba yao kwa kutowasilisha bidhaa au kutoa huduma iliyokusudiwa kwa visingizio mbalimbali.

“Kwa mfano kuna mzabuni mmoja (jina limehifadhiwa) alishinda tuzo ya kusambaza bidhaa katika moja ya ofisi za Serikali, lakini baada ya kutangazwa hakuweza kutokea ili kusaini mkataba na amekuwa akitoa visingizio mbalimbali ikiwemo bidhaa hiyo kupanda bei” Alisema.

Mhandisi Suluo amesema kuwa kitendo cha Wazabuni kutosimamia tuzo wanazopewa kupitia zabuni za umma inazigharimu taasisi nunuzi kwa kuwapelekea kutumia muda na gharama nyingine kuendesha zoezi la kutangaza zabuni upya na kurudisha nyuma mchakato mzima wa kupata mzabuni mwingine. Akieleza athari ambazo wazabuni wanaweza kupata kwa kushindwa kutekeleza tuzo hizo, Mhandisi Suluo amesema ni pamoja na kufungiwa kushiriki katika zabuni za umma.

Kwa mujibu wa Sheria ya Ununzi wa Umma, Kifungu cha 62 (3) (c) sura ya 410 Toleo la Mwaka 2022 sambamba na Kanuni ya 93 (3) (c) ya Kanuni za Ununzi wa Umma zinaeleza wazi kuwa, mzabuni kushindwa kuwasilisha zabuni kwa mujibu wa mkataba kunamtia hatiani kwa kufungiwa kushiriki zabuni za umma kwa kipindi kisichopungua mwaka mmoja na kisichozidi miaka mitano.

Matukio ya baadhi ya wazabuni kutotekeleza mikataba ya zabuni yameonekana kujirudia mara kadhaa licha ya walengwa kuchukuliwa hatua za kisheria, suala linaloathiri utendaji kazi katika uendeshaji wa michakato ya utoaji zabuni za umma kwa kule kupelekea kwake kurudiwa upya kwa mchakato ili kutafuta mzabuni mwengine.

Post a Comment

0 Comments