Ticker

6/recent/ticker-posts

WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA WAKUTANA NA WAKUU WA SHULE ZA SEKONDARI ZA UFUNDI

Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia imekutana na wakuu wa shule za sekondari za ufundi pamoja na taasisi zinazotoa mafunzo ya amali kwa majadiliano katika kuanza maandalizi ya utoaji wa mafunzo amali katika shule hizo mitaala itakapo pitishwa.

Akizungumza katika kikao hicho mjini Morogoro Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema kuwa maoni yaliyotolewa na wadau katika mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 na maboresho ya mitaala wamependekeza wanafunzi wanapomaliza darasa la saba, kidato cha nne, cha sita na chuo kikuu wawe na ujuzi utakaowawezesha kuwa na umahiri.

Prof. Nombo ameongeza kuwa “mitaala ya awali haikuwa na mafunzo ya Amali kwa kiasi kikubwa lakini katika mapendekezo ya maboresho ya sasa, mitaala hiyo imejielekeza kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha na kuongeza fursa za amali mbalimbali kwa kuzingatia mahitaji ya kujiajiri na kuajiriwa. Hivyo, kikao hiki na Walimu Wakuu wa Shule zetu zinazotoa mafunzo ya ufundi(amali) ni muhimu katika kufahamu hali halisi ya miundombinu ya shule hizo kwa lengo la kuweza kazi iliyo mbele yetu”.

Vilevile, aliwaeleza Walimu Wakuu na Wakuu wa Taasisi waliohudhuria kikao hicho kuwa “ni maelekezo ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba ni lazima wahitimu wetu wawe na ujuzi wa kujitengemea. Hivyo, mabadiliko yaliyofanyika kwenye Mtaala ni kuhakikisha kwamba katika ngazi zote za elimu Wanafunzi wanapata ujuzi au amali, Katika kutekeleza maelekezo hayo pamoja na maoni ya wadau, sekta ya elimu imeona ni vyema kuingia katika hatua za utekelezaji wa Mitaala hiyo, alisema Prof Nombo.

Aidha Prof. Nombo amewataka Walimu Wakuu, Wazazi pamoja na wanafunzi ambao watasoma fani za amali katika shule hizo watambue hawatakuwa na muda mwingi sana madarasani bali watakuwa na muda mwingi katika Karakana, au Shambani kwa lengo la kuweza kujifunza kwa vitendo ili kutoka na Amali zitakazomuwezesha kufanya kazi.

Wazazi watambue kuwa huu ni mwelekeo mpya wa Kielimu ambapo tunataka kutoa watanzania ambao wanauwezo wa kufanya kazi tofauti na ilivyokuwa zamani, walikuwa wana ujuzi wa nadharia sasa tunatamani wawe na ujuzi wa nadharia kidogo na ujuzi wa kufanya kazi kwa wingi, alisema Prof Nombo.

Kwa upande wake mmoja ya wakuu wa shule kutoka Shule ya Sekondari ya Wavulana Bwiru Mwalimu Thomas Werema ameishauri Serikali kuwa ili kuhamasisha watoto wengi kujiunga na shule hizo, ni vema kuwapatia dhana za kufanyia kazi wanafunzi wanaofanya vizuri wanapomaliza mafunzo ya amali ili wanapohitimu waweze kujiendeleza zaidi.

Aidha, Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya ufundi Ifunda Mwalimu Yona Mwakalango ameishauri Serikali kutoa elimu zaidi kwa Walimu na Wazazi ili waweze kuhamasisha watoto wao kusoma katika Vyuo vya Ufundi lakini pia ameiomba Serikali kuendeleza vipaji vya watoto vinavyotambuliwa shuleni ili Teknolojia wanazozigundua ziweze kuwa na manufaa katika jamii.

Post a Comment

0 Comments