Ticker

6/recent/ticker-posts

ZAIDI YA PROGRAMU 300 ZA MAFUNZO ELIMU YA JUU KUANZISHWA


Zaidi ya programu 300 za mafunzo elimu ya juu kuanzishwa ama kuhuishwa ili kuendana na Dira na Mipango ya Maendeleo ya Taifa sambamba na mahitaji ya sasa ya kijamii, kiuchumi na soko la ajira.

Hayo yamesemwa Bungeni Juni 8, 2023 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti maalum Mhe. Nusrati Shaaban Hanje aliyetaka kujua ni lini Serikali itapitia mitaala ya Vyuo Vikuu ili kufungamanisha elimu sambamba na dira na mipango ya maendeleo ya Taifa.

Prof. Mkenda amelieleza Bunge kuwa tayari Vyuo Vikuu vya Serikali na Binafsi kupitia mradi wa Higher Education for Economic Transformation - HEET vimepata mafunzo mbalimbali ya kuandaa programu zinazoendana na vipaumbele vya nchi na mahitaji ya soko la ajira

“Tayari Wizara yangu imeshatoa maelekezo kwa Vyuo Vikuu kuhuisha na kufanya maboresho ya mitaala yao yote ili iendane na Dira na Mipango ya Maendeleo ya Taifa ambayo kwa sasa inalenga kutoa Elimu itakayompa kijana wa Kitanzania elimu na ujuzi kwa mujibu wa mahitaji ya sasa,”amesema Prof Mkenda

Prof Mkenda ameongeza katika kutekeleza hilo Vyuo vimeunda Kamati za Ushauri wa Insia (Industrial Advisory Committees -IACs) zenye wajumbe kutoka Sekta za Waajiri kwa ajili ya kutoa ushauri kwa taasisi hizo juu ya programu zinazoendana na soko la ajira.

Post a Comment

0 Comments