Ticker

6/recent/ticker-posts

BRELA , COSOTA, BPRA, COSOZA WASAINI MAKUBALIANO YA USHIRIKIANO

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imesaini makubaliano ya ushirikiano baina yake na Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA), Ofisi ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali Zanzibar (BPRA) na Ofisi ya Hakimiliki Zanzibar yenye lengo la kutekeleza mradi wa Kituo cha Mafunzo ya Miliki Ubunifu nchini.

Hayo yamejiri leo Julai 21, 2023 mbele ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana katika hafla ya ugawaji Mirabaha kwa wabunifu iliyofanyika kwenye Hoteli ya Hyatt Regency, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa amebainisha kuwa Serikali inatambua uhitaji mkubwa wa elimu na mafunzo kuhusu Miliki Ubunifu ili kuhakikisha kuwa bunifu zinaendelea kufanyika, zinalindwa na zinaingiza kipato stahiki kwa wabunifu.

“Uanzishwaji Kituo cha Mafunzo ya Miliki Ubunifu hapa nchini ni dhamira ya dhati ya Serikali katika kuhakikisha wabunifu wananufaika na kazi zao lakini pia zinalindwa. Mafunzo haya yatatolewa kwa wasanii, waandishi na wabunifu wote katika masuala ya Hakimiliki na masuala ya Miliki Ubunifu kwa ujumla", amesema Bw. Nyaisa.

Awali BRELA kama ofisi ya Miliki Ubunifu kwa kushirikiana na COSOTA, COSOZA na BPRA ziliwasilisha maombi kwa Shirika la Miliki Ubunifu Duniani (WIPO) ya uanzishwaji wa kituo hicho cha mafunzo.

Bw. Nyaisa ameongeza kuwa kwa sasa Tanzania na WIPO zinafanya utaratibu wa kufanya tathimini ya mahitaji nchini na pia katika utekelezaji wa mradi huu taasisi zinazosimamia masuala ya Miliki Ubunifu zitatoa wataalam ili kuwezesha utoaji wa mafunzo husika.

Amewapongeza wabunifu wote kwa kuendelea kufanya kazi na kubuni kazi mbalimbali za ubunifu katika Sanaa na kazi za maandishi na kuhakikisha kuwa wanajipatia kipato wao na taifa kwa ujumla.

Utolewaji wa mafunzo haya nchini Tanzania utasaidia kuhamashisha wabunifu kufanya bunifu nyingi zaidi, kuipandisha Tanzania kwenye ramani katika masuala hayo na kuwa chachu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Godfrey Nyaisa ( wa pili kushoto), Kaimu Mkurugezi wa Ofisi ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali Zanzibar (BPRA), Bw. Rashid Masoud Othman ( wa tatu kushoto), Afisa Mtendaji Mkuu Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA), Bi. Doreen Sinare (wa tatu kulia) na Mkurugenzi wa Idara ya Leseni, Ukaguzi na Ugawaji Mirabaha Taasisi ya Hakimiliki Zanzibar (COSOZA), Bw. Muumin Mwinyi Mzee ( wa pili kulia) wakionesha mikataba ya makubaliano ya ushirikiano yenye lengo la kutekeleza mradi wa Kituo cha Mafunzo ya Miliki Ubunifu nchini. Hafla hiyo imefanyika tarehe 21 Julai, 2023 jijini Dar es Salaam.
Afisa Mtendaji Mkuu wa COSOTA Bi. Doreen Sinare akikabidhi Leseni kwa Kampuni Binafsi ya Wasanii wa Muziki ya Kukusanya na kugawa Mirabaha - TAMRISO Julai 21, 2023 Jijini Dar es Salaaam wakati wa Hafla ya Ugawaji wa Mirabaha kwa Wasanii.

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma alishuhudia tukio hilo.

Post a Comment

0 Comments