Makamu wa Rais Dk.Philip Mpango( wa pili kushoto) akikabidhi mtungi wa Oryx Gas mkazi wa Buhigwe mkoani Kigoma Aisha Nduhiye (kulia) wakati wa tukio la ugawaji wa vifaa mbalimbali ikiwemo mitungi na majiko ya oryx kwa wanawake wajawazito pamoja pamoja na wahudumu wa sekta ya afya. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Doris Mollel Foundation inayoshughulika kusaidia Watoto Njiti aliyepeleka vifaa
Makamu wa Rais Dk.Philip Mpango (katikati) akipiga makofi kuwapongeza Kampuni ya Oryx Gasi Tanzania kwa jitihada wanazofanya katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kugawa bure mitungi ya gesi ya Oryx kwa wananchi
****************
Na Mwandishi Wetu
MAKAMU wa Rais Dk. Philip Mpango, amesema kwamba juhudi za kulinda mazingira zinazofanywa na taasisi mbalimbali kuhamasisha nishati safi ya kupikia zinastahili kuungwa mkono na wananchi wote.
Aidha ameipongeza Kampuni ya Oryx Gas Tanzania Limited kwa kazi nzuri inayoifanya kuiwezesha jamii kupata gesi safi ya kupikia, hivyo kutekeleza mkakati wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Dk. Mpango ameeleza hayo mbele ya wananchi wa Wilaya ya Buhigwe, mkoani Kigoma wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa mbalimbali kwa wanawake wajawazito pamoja na wahudumu wa afya katika Wilaya ya Buhigwe ambavyo vimetolewa na wadau kupitia Taasisi ya Doris Mollel Foundation.
Katika ugawaji huo wa vifaa , Makamu wa Rais Dk.Mpango aliyekuwa mgeni rasmi alikabidhi mitungi hiyo kwa wanawake wajawazito pamoja na watoa huduma za afya ambapo wajawazito 214 na watumishi wa afya ngazi ya jamii 86 katika Wilaya hiyo na kufanya jumla ya mitungi 300 kutolewa bure.
Pamoja na mambo mengine Dk.Mpango ameipongeza kampuni hiyo kwa kazi nzuri inayoifanya kwa kuiwezesha jamii kupata gesi safi ya kupikia hatua ambayo inastahili kuungwa mkono katika harakati za kutunza mazingira.
Amewahimiza wanachi wa Buhigwe kutumia gesi ya Oryx kwa kuwa kampuni hiyo inasaidia jamii kwa kutoa bure mitungi na majiko.
Awali Meneja Mkuu wa Oryx Gas Kanda ya Kaskazini, Alex John, alisema kampuni hiyo ikiwa kinara wa soko katika usambazaji wa gesi ya kupikia nyumbani (LPG) nchini, inaendelea kufanya uwekezaji mkubwa kwa wananchi kuunga mkono juhudi za serikali za kuhimiza matumizi ya nishati hiyo.
Amesema gesi safi ya LPG ni suluhisho la kutokomeza matumizi ya kuni na mkaa, hivyo kuboresha afya ya jamii, ustawi na utunzaji wa mazingira, pia ni utekelezaji wa agizo la Rais Dk. Samia Suluhu Hassan la kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia kama mkakati wa kulinda mazingira.
Ameongeza kabla ya ugawaji wa majiko na mitungi hiyo, yalitolewa mafunzo kuhusu matumizi sahihi ya gesi yaliyowezeshwa na meneja mkuu huyo wa kanda ya kaskazini.
“Tunaamini wahudumu wa afya wa wilaya ya Buhigwe wanawakilisha watu wengi na wanapaswa kuwa mfano wa mabadiliko ya nishati safi.
“Sote tunajua kuwa kundi hili lina ushawishi mkubwa kwa watu wanaowahudumia, hivyo Oryx tumeamua kutoa mitungi hiyo na majiko ya gesi ya LPG kuwahimiza na kuwashawishi wengine kuhusu umuhimu wa mabadiliko ya nishati ya LPG,” amesema.
0 Comments