Na Mwandishi Wetu,- Kigoma
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM)Daniel Chongolo amesema Chama hicho kinaelekeza Serikali kuisukuma na kuongeza spidi katika kuhakikisha mjadala wa uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam unafika mwisho ili wananchi waanze kuona matokeo yake.
Chongolo ameyasema hayo leo Julai 26,2023 wakati akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Kigoma kupitia mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Mwanga Center ambapo ametumia nafasi hiyo kuitaka Serikali isiingie kwenye maneno ya siasa na badala yake wasimame kwenye hoja na hatimaye bandari iongeze ufanisi.
"Tunanachotaka ni kuona bandari inaongeza ufanisi,inaletea matokeo na inachangia pato kubwa la Taifa na kuongeza tija kwa nchi ya kuwahudumia Wananchi na sio vinginevyo.Mambo yote ya maneno maneno,siasa hizi tusizipe nafasi.
" Sisi ndio tumepewa dhamana ya siasa,sisi tunakuja kuzungumza na wanasiasa wenzetu na Watanzania waliotupa dhamana,Serikali mambo yao ni ya kutenda na kuleta matokeo,na wasifanye mchezo hata kidogo kutosimamia maslahi ya nchi kwa kila wanachokifanya’’,amesema Chongolo.
Aidha Chongolo alieleza hatua kwa hatua kuhusu uamuzi wa Serikali kuingia makubaliano ya uwekezaji wa kuboresha uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam huku akifafanua lengo kuu ni kuhakikisha bandari hiyo inatoa huduma kwa ufanisi mkubwa.
0 Comments