MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu amekabidhi vitendea kazi vyenye thamani ya Sh Milioni 6.9, kwa watendaji wa Chama ngazi ya Wilaya,Kata na Matawi kwenye jimbo lake ikiwa ni mchango wake katika kutunza kumbukumbu za vikao vya Chama na wanachama kwenye ngazi zote.
Akikabidhi msaada huo Julai 15,2023,mbele ya Kamati ya Siasa ya wilaya,Mtaturu amesema anatambua kazi kubwa inayofanywa na chama chake katika ngazi zote ndio maana ameamua kutoa msaada huo.
"Natambua uhai wa Chama ni vikao,hivyo vitendea kazi hivi nilivyogawa vitasaidia kutunza kumbukumbu za vikao hivyo katika ngazi zote za uongozi,"amesema.
Akipokea vifaa hivyo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM ),wilaya Mika Likapakapa amemshukuru Mbunge Mtaturu kwa kujitolea mara kwa mara kukisaidia chama.
"Hivi karibuni Mbunge huyu alituchangia vifaa vya ujenzi Gypsum Board 75,Saruji mifuko 40,mbao za kuweka dari kwenye ukumbi wetu uliopo kwenye ofisi ya CCM Wilayani hapa, huu ni moyo mkubwa sana tunamshukuru na kumpongeza sana,"amesema.
Amesema Chama kinatambua na kuthamini mchango wake na kumuomba aendelee na kazi hiyo njema huku akiwaasa wanachama na wananchi waendelee kumuunga mkono.
0 Comments