*Asisitiza CCM haina muda wa kujibu lugha za matusi, wao wanaongoza nchi
Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV –Arusha
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Daniel Chongolo amesema kwanini watanzania wawe na shaka na maono ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu uwekezaji unaotaka kufanywa katika bandari ya Dar es Salaam wakati maono kama hayo yamefanya vizuri katika filamu ya Royal Tour na utalii umejibu.
Chongolo ameyasema hay oleo Julai 22,2023 alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika jijini Arusha na kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi kutoka mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara ambapo pamoja na mambo mengine alielezea dhamira ya Serikali katika uwekezaji wa bandari hiyo ukiwa na lengo la kuongeza wigo wa ukusanyaji wa fedha ambazo zitatumika katika kutatua changamoto za wananchi.
“Moja ya kazi ya msingi ya Serikali ni kukusanya fedha na kutafuta fedha za kutekeleza na kutatua changamoto za wananchi, kazi ya serikali sio kupiga makofi , kushangilia, kazi yake ni kutatua changamoto na ili utatue changamoto lazima utengeneze uhakika wa mapato, ili uwe na uhakika wa kutatua changamoto lazima uwe na fungu la kutosha kufanya hivyo.
“Nimesema hapa kwa kutaja barabara zitakazojengwa mkapiga makofi , fedha zinazotakiwa kujenga hizo barabara ni zaidi ya Sh.Trilioni 3.7. Fedha hizi usipokuwa nazo utabaki na ahadi isiyotekelezeka kwa muda mrefu, Serikali makini haikai kushangaa bali inatafuta namna sahihi ya kwenda kutafuta fedha za kutatua changamoto,”amesema.
Amefafanua ndio maana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutambua bila fedha hawezi kufanya mambo alifikiri na kubuni na kuja na mpango wa kutangaza utalii wa nchi hii kupitia Royal Tour na wakati anapita huko porini kila siku kurekodi ile filamu kwa ajili ya hayo matangazo watu walimbeza wakaona kama anachokifanya hakina maana.
“Leo ninyi wote ni mashahidi , hivi ni wangapi wanapeleka salamu za kumshukuru baada ya filamu ya Royal Tour kujibu? Leo wanaonufaika ni wenye magari ya utalii ni Mama Samia ? Wenye hoteli zinazolaza watalii ni Rais Samia ? Na wale wanaondesha magari wakitoka kule na noti mfukoni wakija wanakuja kununua bidhaa kwenye maduka yetu wanaonufaika ni Rais Samia?
“Ni sisi, tunaona ni jambo la kawaida kwasababu imekaa vizuri, hatukumbuki kama kuna mtu alikesha akabuni,akamua, akachukua hatua ya kutekeleza kufanya matangazo kwa ajili ya kutangaza utalii wa nchi yetu leo tunaonufaika tunakula kiulani hatumkumbuki, hatufikirii , tunamlundukia jambo jipya sisi tunakula starehe, hatutendi haki
“La utalii limetiki sasa tumekwenda kwenye bandari , kelele zao mnazisikia hamzisikii ? kama alikuwa na maono kwenye Royal Tour na utalii umejibu mashaka ya Bandari yanatoka wapi ? Walionitangulia wameeleza kwa kina kuhusu makubaliano ambayo tumeingia na Serikali ya Dubai.Sitaki kurudi huko.”
Ametumia nafasi hiyo kueleza kuhusu upotoshaji kuhusu bandari ulipoanza mpaka ulipofikia , mwanzo wapotoshaji walikuja wakasema bandari imeuzwa kwa miaka 100 , walipoona jambo hilo lina majibu na limejibiwa wakabadilisha wakasema shida ni uwekezaji hivyo waachane na uwekezaji.
“Walipoona tumewajibu na kuwaambia uwekezaji ni muhimu hakuna anayerudi nyuma tunasonga mbele kama mna kipengele mnachangamoto leteni tujadili tukiweke sawa tusonge mbele tukiwa na mkataba ambao ninyi mtaona unafaa na sisi tutaona unafaa mpaka leo hakuna aliyeleta mapendekezo, wanazunguka tu
“Wameenda mbali wamekosa hoja sasa wameamua kuanza kutukana , sasa mtu akishakosa hoja akaanza kutukana na sisi ni waungwana tunadhamana ya kuwahudumia watanzania tukiingia kuanza kutukana itakuwa kituko, tuna wajibu wa kuongoza nchi, kazi ya kuongoza ya nchi sio lele, mama lazima tukae mguu sawa, lazima tuwe timamu kuhakikisha tunatatua changamoto za watanzania.
“Hatuko kutukanana wala kujibu upuuzi, tupo kutibu changamoto na kutatua changamoto za wananchi.Lakini ukiona hutukanwi ujue hufanyi wewe ukitaka usitukanwe jifungie ndani lala , ukitaka usitukane nenda tu kawe mtu hohe hahe , wewe si asubuhi si mchana upo nani atakutukana…
“Kwasababu huna cha kutukaniwa, sisi tunawajibu wa kufanya matusi, kebehi na maneno yote ya dharau tunayakaribisha ni haki yetu kwasababu tunafanya. Kazi ya kuongoza nchi ni kazi kubwa , kazi ya kutunaka ni rahisi , kazi ya kumfanya mtanzania kuwa na uhakika wa afya, mtoto kusoma, uhakika wa barabara , mlo wake sio kazi ya lele mama ni kazi kubwa ni kazi inayokutaka uwe sawa sawa.
0 Comments