Ticker

6/recent/ticker-posts

WMA WAJA KIVINGINE KUTATUA CHANGAMOTO KWA JAMII

Wakala wa Vipimo nchini (WMA) wamekuja kisasa zaidi ili kuhakikisha wanatatua changamoto mbalimbali katika jamii ya Kitanzania na kuhamasisha utumiaji wa vipimo sahihi wakati wote.

Akizungumza katika Maonesho ya 47 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala huo, Stella Kahwa amesema WMA imekuja na bidhaa muhimu katika kuhakikisha jamii ya Watanzania inafurahia na kufaidika na matumizi ya vipimo sahihi kama watakavyo Shirika la Vipimo Duniani.

“Wakala wa Vipimo sasa tumeingia kwenye Gesi Asilia, tunahakikisha matumizi sahihi ya vipimo katika Gesi Asilia ambayo imekuwa ikitumika sana katika shughuli mbalimbali za kibinadamu, na hii ndio kazi yetu sisi WMA, siku zote tunahimiza na kuhakikisha matumizi bora ya vipimo,” amesema Kahwa.

Pia, Kahwa amesema Wakala wa Vipimo kwa sasa umeingia kwenye vifaa vya kupima sauti kwenye kumbi za starehe na baadhi ya sehemu za ibada ili kutatua changamoto kwa jamii, baada ya kuwepo malalamiko ya uwepo wa sauti kubwa katika makazi ya watu.

“Mfano sasa hivi, kumekuwa na malalamiko kuhusu kelele kwenye baadhi ya kumbi za starehe sehemu mbalimbali nchini, sisi na wenzetu, Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) katika kuhakikisha tunakuwa na vipimo sahihi wa vifaa hivyo vya kupima sauti katika sehemu hizo za starehe,” ameeleza Kahwa.

Vile vile, amehimiza Watanzania hususani Wafanyabiashara, Wajasiriamali na watumiaji wengine wa vipimo, wahakikishe wanatumia vipimo hivyo sahihi ili kuhamasisha ushindani wa bidhaa zao ambazo wanazalisha na kuzipeleka kwa jamii kwa matumizi. WMA imetoa namba ya bure: 08110097 ili kupata elimu zaidi kuhusu vipimo.






Post a Comment

0 Comments