Kamati ya Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeridhishwa na utendaji kazi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kuendelea kusimamia vyema rasilimali za misitu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe. Timotheo Mnzava (Mb) ameyasema hayo leo katika kikao cha Kamati hiyo kilichofanyika ukumbi wa Utawala Annex Bungeni jijini Dodoma.
Mhe. Mnzava amewapongeza wahifadhi kwa kujitolea kufanya kazi kwa bidii.
"Tuwatie moyo hawa wapiganaji wetu kwani wameendelea kutekeleza majukumu yao vyema na kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa, waendelee kuitumikia nchi kwa kuwa wanajitolea na sisi kama Bunge tunawaunga mkono" Mhe. Mnzava amesisitiza.
Aidha, ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kufanyia kazi mapendekezo ya wajumbe wa Kamati hiyo na kuangalia namna bora ya kuzuia ukataji wa miti kwa kuwa yapo maeneo ambayo wananchi wanaishi kwa kutegemea miti hiyo .
Naye, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) ameishukuru kamati hiyo kwa mapendekezo na kuahidi Serikali itafanyia kazi.
Pia, amefafanua kuwa Serikali inaendelea kuhamasisha wananchi kuacha kukata miti hovyo pamoja na kuacha matumizi ya nishati chafu na badala yake kutumia nishati safi.
Kikao hicho kimehudhuriwa na baadhi ya Watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
0 Comments